PICHA ya Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Leonidas Gama, iliyochapishwa hivi karibuni kwenye vyombo vya
habari ikimuonesha akilia mbele ya mali za mwekezaji zilizoharibiwa na wafugaji
sikuipenda.
Kwenye Kaya yangu hasa eneo
analotawala mkuu huyo wa mkoa kumekuwa na matukio mengi ya mauaji ya wananchi yanayosababishwa na
mgogoro wa ardhi baina ya wawekezaji, serikali na wafungaji; sote tunajua!
Hakiyamungu sijawahi kumuona mkuu huyo wa mkoa akilia
mbele ya maiti ya mfugaji hata mmoja. Nilichokiona juzi nilistaabu na kujiuliza
kulikoni mkuu mwenzangu alilie mali za mwekezaji kuliko uhai wa wananchi anaowaongoza?
Mambo yako wazi; mgogoro kati ya
Kampuni ya Kitalii ya Tanganyika Film Safary iliyochomewa mali zilizomliza mkuu
wa mkoa dhidi ya wafugaji wa Kijiji cha Miti Mirefu wilayani Siha, Gama anaujua,
lakini fikra kuwa ameshawahi kulia kuutatua haipo.
Kiongozi wa wafugaji wa Miti
Mirefu, Kitasho Simeli amenukuliwa mara kadhaa akilalamika wachungaji kupigwa
risasi na askari wa wanyamapori na maiti zao kutelekezwa porini bila serikali
kuchukua hatua jambo linalochangia wananchi kuingiwa na hasira.
Hii ndiyo aina ya wakuu nilionao
kwenye Kaya yangu, wanapolalamika wananchi wazalendo kufanyiwa unyama na hao
tunaowaita wawekezaji hakuna kiongozi anayekuwa mkali; wanamaslahi binafsi
sijui. Cha kujiuliza kwa nini walilie mali na siyo uhai wa watu?
Maana tungekuwa na uchungu na
maisha tungelinda zaidi uhai wa watu kuliko mali. Mwekezaji anapoharibiwa mali
zake si jambo la kumfanya mtu atoe machozi na kuacha kufanya hivyo anapoona
maiti zimesambaa msituni huku kisa kikitajwa kuwa ni mgogoro wa ardhi.
Nimpe taarifa Gama na viongozi
wengine wa kaya hii, mali anazozililia zina mbadala wake, mhusika atalipwa bima
na fidia nyingine na maisha yataendelea, lakini uhai wa watu utarejeshwa kwa
njia gani? Fikra pevu zinahitajika kujua hili.
Hatuwezi kuwa na taifa lenye
viongozi wanaolilia mali na kuacha kulilia uhai ambao ni haki ya kikatiba ya
wananchi. Hatuwezi kuwa na wakuu wanaoumizwa zaidi na uharibifu wa mali za
wageni zaidi ya mali za wazawa. Hatuwezi pia kujenga taifa lenye usawa kama
tutathamini mali za wawekezaji zaidi ya mali za wananchi wetu.
Tunawezaje kusema tunawatumikia
wananchi kwa usawa kama hatuumizwi na vifo vya ng’ombe wao wanaokosa malisho
wanayoyadai kila mara bila kuwapatia ufumbuzi madai yao na wakati huohuo
tukaonesha upendeleo wa wazi kwa wageni?
Mkuu wa Kaya siwezi kukubaliana
na hali hii kwamba niwaache wakuu wa mikoa walilie mali za wawekezaji na
wasifanye hivyo kwenye vifo vya ng’ombe wa wafugaji ambao kwa tafsiri yetu hiyo
ni pia ni mali sawa na magari ya Tanganyika Film Safary yaliyochomwa moto.
Ni lazima mimi kama Mkuu wa Kaya
nisimamie mageuzi ya ufahamu, niongoze mfumo mpya wa kuongoza wananchi kwenye
kaya hii ili mambo yasiendelee kwenda mrama.
Miaka nenda rudi migogoro ya
wakulima na wafugaji inaendelea, watu wanakufa kila mahali katika kaya hii,
mwitio wenye utashi kwa viongozi haupo!
Hivi tunashindwaje kutenga maeneo
ya malisho na kilimo kwenye nchi kubwa kama hii? Hii ni aibu ya viongozi.
Ni ugumu gani uliopo wa kumaliza
tofauti kati ya wawekezaji na wafugaji hasa kwenye maeneo ya hifadhi
tulizozitengea sheria za kitalii. Hili halitutoi machozi ila tukiona mali
ambazo siyo zetu majozi waaaaa! Ni aibu kubwa!
No comments:
Post a Comment