Maisha ya
shule yana mapito mengi. Kubwa katika yote ni kupevuka ufahamu. Ni ukweli
usiopingika kuwa, kadiri mwanafunzi anavyozidi kujifunza uwezo wake wa kufikiri
unakua na hivyo kumpa changamoto pana zaidi za kukabiliana na maisha.
Unapozungumzia
vikwazo vya kimasomo lazima mchanganuo wa umri na ngazi za madarasa uzingatiwe
ili mantiki niliyosema iwe na maana. Upo
utofauti kati ya vikwazo vya mwanafunzi wa chekechea na yule wa shule ya
msingi, sekondari au chuo.
Msingi; ni
ukubwa wa ufahamu. Mahali ambapo mtoto wa shule ya awali asipoweza kutambua
tatizo la fedha ya matumizi shuleni, ulinganifu hauko hivyo kwa mwanafunzi wa
chuo ambaye anatakiwa kujitegemea kwa kila kitu.
Kama nilivyosema,
kadiri unavyoelimika, unauongezea ubongo kazi ya uchambuzi. Ukubwa wa ufahamu
utakufanya uwe mdadisi wa kila kitu na hivyo kujiweka katika hatari ya kupata
msongo wa mawazo.
Wanasaikolojia
wameshindwa mara nyingi kuuzungumzia msongo wa mawazo mazuri kwa sababu hauna
hasara za moja kwa moja, badala yake wametazama zaidi msongo wa mawazo yanayoumiza
ambao hushambulia vichocheo vya uelewa na hivyo kumfanya mtu ashindwe kupata
msaada wa fikra kutoka kwenye akili yake.
Uchunguzi
unaonesha kuwa, wanafunzi wengi wameshindwa kufanya vizuri kimasomo kutokana na
tatizo kuu la msongo wa mawazo yanayoumiza. Mfano kuachwa kimapenzi,
kusalitiwa, kufiwa na walezi au wazazi, kukabiliana hali ngumu ya kimaisha au
kukosa msaada juu ya matatizo fulani.
Mwanafunzi
yeyote hata mwenye akili ya miujiza akiruhusu msongo wa mawazo hawezi kufaulu
mitihani, hawezi kufanya vizuri kimasomo, atajikuta anaporomoka na kuishia
pabaya.
Pengine
kutokana na nafasi niliyonayo kwenye safu hii, nijibu swali mwanafunzi afanye
nini kukabiliana na kikwazo hiki cha msongo wa mawazo?
Kwanza, ni
kukubali kupokea tatizo. Watu wengi wanaumizwa na mawazo kwa sababu wanadhani
hawastahili kupata tatizo husika. Changamoto yoyote inayokupata ipokee kwanza
halafu itafutie ufumbuzi kwa kuwashirikisha watalaamu wa masuala ya saikolojia,
rafiki au ndugu wenye uelewa wa kutosha, huku wewe mwenyewe ukipuuza ukubwa wa
tatizo.
Kwa msaada zaidi tembelea blogu
yangu ya www.richmanyota.blogspot.com
No comments:
Post a Comment