Wednesday, April 7, 2010
HATUA KUMI ZA KUCHAGUA MCHUMBA
Wengi wamejikuta wakiitwa wahuni kutokana na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na makundi ya wanaume au wanawake. Hata hivyo wachunguzi wa masuala ya mapenzi wanasema idadi kubwa ya wapenzi si kigezo sahihi cha kupima tabia ya mtu na kumhusisha na uhuni.
Watalaam hao wanataja safari ya kupata chaguo halisi la mwanaume/mwanamke wa maisha ndiyo inayowaponza wengi kiasi cha kujikuta wameingia katika kashfa ya kuwa na uhusiano na dazeni ya wapenzi.
Wanasema msichana/mvulana anayeingia katika uwanja wa mapenzi kwa kuwa na hisia za kufanya ngono, hukosa umakini wa nani anafaa kuwa mpenzi wake kutokana na kukosa elimu ya uhusiano kutoka kwa wazazi wake.
Kwa mantiki hiyo, bila upembuzi wa kina, mtu asiye na elimu ya jinsi ya kumpata mpenzi wa kweli hujikuta ameangukia kwa mwanaume/mwanamke asiyemfaa, ambapo baadaye huamua kuachana na huyo na kwenda kwa mwingine kujaribu bahati tena ya kupata penzi la kweli.
Zinatajwa zawadi, hitaji la kusaidiwa kimaisha, mvuto wa kimahaba na mazoea kuwa ni vichocheo vinavyowaangusha wengi kwenye mapenzi na wasiowafaa.
Ukweli ni kwamba mtu aliyenaswa kwa ‘ujinga’, huwa hakatwi kiu ya penzi na mwanaume/mwanamke asiye chaguo sahihi la maisha yake. Hivyo hufikia maamuzi ya kujiingiza katika uhusiano mpya mara 2,3,4,5 na kujikuta wakiambulia wanaume/wanawake wale wale wasio sahihi kwake.
Mwanamnke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Suzzy aliwahi kuniomba ushauri, akasema amechoka kuchezewa, maana kila mwanaume anayempata anakuwa si chaguo lake. Lakini kibaya zaidi kuachia ngazi au kutemwa huku akiwa tayari ameshafanya mapenzi na wanaume hao.
Nia ya swali lake ilikuwa ni kuniomba njia za kumtambua mwanaume mkweli bila kufanya naye mapenzi? Aliuliza hivyo huku akiwa na hoja kuwa wanaume wengi hawako tayari kuwa na uhusiano na msichana bila kufanya naye mapenzi na wakati huo huo huficha tabia zao chafu wakilenga kumnasa wamtakaye.
Binafsi nafahamu kuwa kuna wanawake/wanawake wengi ambao hujiingiza katika mapenzi kwa kutekwa na hadaa za mwili na kujikuta wanacheza mchezo wa kitoto wa pata potea.
Ni madhumuni ya somo hili kufundisha vigezo vya kumpata mwanaume/mwanamke halisi wa maisha, bila kufanya naye mapenzi. Njia hii ina faida kwa pande zote mbili yaani kwa mwanamke na mwanaume kwani kuacha au kuachwa bila kufanya mapenzi ni bora kuliko kuwa muonjaji, tabia ambayo huathiri kisaikolojia na ni hatari kwa afya.
Ifuatavyo ni njia ya kisaikolojia ambayo mwanamke anaweza kutumia kumpata mwanaume mwenye kumfaa bila kufanya naye mapenzi tena ni jibu sahihi la kuondokana na mchezo wa kubahatisha kwa wanaume wanaosaka wapenzi wa kweli na si taksi bubu ambazo mchana huweka namba za njano usiku nyeusi.
KWANZA- Ni ya mwanamke/mwanaume mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi anayemhitaji katika maisha yake. Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake na kila mwanamke anaye wake wa maisha pia. Hivyo asiyekufaa wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe kujitambua kwanza ili umtambue umtakaye.
Wanawake/wanaume wengi hawafahamu wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi, wakachezewe na kuumizwa moyo bure.
PILI- Ni kuketi chini na kuorodhesha vigezo stahili vya mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, ana upungufu wake.
TATU- Anza kumsaka kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako hutambulika kwa moyo kurithika na mwili kusisimka.
NNE - Kuanzisha safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.
Katika uchunguzi huu mwanamke/mwanaume anayetafuta mpenzi hana budi kupitia na kumlinganisha huyo aliyempata na vigezo alivyojiwekea. Zoezi hili liendane na kuweka alama ya pata kila anapobaini kuwa mwanaume/mwanamke anayemchunguza amepata moja ya vigezo vyake. Lakini pia aweke alama ya kosa kwa kila kasoro anayoivumilia na ile asiyoivumilia.
TANO - Ajipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza huyo mwanaume, kisha aketi chini na aanze kujumlisha alama za vigezo alivyovijiwekea na jinsi mwanaume huyo alivyopata au kukosa.
Ikibainika mwanaume aliyechaguliwa amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo vilivyowekwa, basi ujue kuwa anafaa. Kuhusu alama chache alizikosa anaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati wa maisha ya ndoa.
Lakini angalizo kubwa kabisa ni kwamba mwanaume/mwanamke akionekana kuanguka katika kasoro zisizoweza kuvumilia kwa zaidi ya alama tatu. Yaani kwa mfano ni mlevi, mwizi, muongo, mbishi na katika hizo kashindwa 3, huyu hafai, ni vema akawekwa kando kwani huwezi kubeba kero 3 kwa pamoja katika maisha.
SITA - Kusajili mapenzi yenye malengo yanayotekelezeka. Lazima baada ya kuchunguzana kwa kina wapenzi watengeneze muongozo wa mapenzi yao. Wasiwe kama wanyama, lazima mipango ya wapi wametoka walipo na wanapokwenda.
Hata hivyo watalaam wanasema lazima wapenzi wapime umakini wao kwa vitendo. Kama wamekubaliana kuoana, suala la mume kwenda kujitambulisha kwa wakwe na hatua ya kuiendea ndoa ionekane. Usiri usiwepo tena. Kila mmoja amuone mwenzake kama sehemu ya maisha yake na mara zote wasaidiane kwa ukaribu.
SABA - Ni vema ndugu wakashirikishwa ili kuwapa nafasi na wao ya kuamua kama mapenzi hayo ni budi yakaendelea au yakasitishwa. Ni ukweli ulio wazi kwamba licha ya wengi kupuuza maamuzi ya ndugu kwa madai ya kuwa hawana nafasi kwa wapenda nao, lakini uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi wengi huacha kutokana na sumu za ndugu hasa pale wanapokuwa wameonesha kutounga mkono uhusiano wa wanaotaka kuoana
NANE - Hatua hii ni ya kuweza kuzungumzia ufanyaji mapenzi, hapa nina maana kama wapenzi wamejizuia kwa muda mrefu na wanahisi kuchoka wanaweza kujadiliana kuhusu hilo na kuamua ufanyaji huo wa mapenzi una lengo gani, kama ni kuburudisha miili basi suala la afya na uzazi salama litazamwe.
TISA - Kutimizwa kwa ahadi ya kuoana ni hatua ya tisa ambayo nayo si busara ikachukua muda mwingi kutekelezeka, kwani ucheleweshaji mwingi wa ndoa nao huvunja moyo na mara nyingine umewafanya wengi kutoaminiana.
KUMI - Kuamua kuwa mwili mmoja kwa kuvumilia na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zote za maisha ukiwemo mkwamo na dhiki ambazo huchangia sana ndoa nyingi kuvunjika. Hapa pia ni wajibu wa wanandoa kuchukuliana udhaifu na kusaidia, kuwa tayari kujifunza na kujali zaidi upendo kuliko hisia za mwili ambazo wakati mwingine hudanganya na hivyo kumfanya mwanandoa asivutiwe na mwenzake.
Mwisho ni kwamba kanuni hizi huwafaa watu wazima mapenzi ya kitoto hayawezi kujenga misingi hii imara mara nyingi ni kudanganyana, kuharibiana maisha, kupeana mimba na maradhi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
nashukuru kwa somo lako nimejifunza kitu
ReplyDeletenimeelewa ahsanten
ReplyDeleteje unawezaje kumpata anaekupenda?
ReplyDelete#mimi kunamdada nilikua nampenda ila kachukizwa na maneno ya marafiki zangu nimejalibu malanyingi kumweleza ukweli ila hataki nielewa nifanyeje? naombeni mawazo yenu wadau kupitia email; canord70@gmail.com