Tuesday, May 11, 2010

NJIA YA KUPUNGUZA MAUMIVU WAKATI WA KUJIFUNGUA




Nimewahi kusoma habari za mkunga Kim Hildebrand Cardoso kutoka Berkeley, California nchini Marekani kuhusiana na uchungu waupatao wanawake wakati wa kujifungua na vifo vitokanavyo na uzazi. Ingawa sina cheti cha utabibu niliamua kujikita katika uchunguzi ili nijue kwanini akina mama wengi hasa Tanzania hupata matatizo wakati wa kujifungua?

Nilichogundua ni kwamba karibu kila msichana mwenye umri wa kuweza kubeba ujauzito anatambua matatizo ya mimba na maumivu makali wakati wa kujifungua, lakini miongoni mwa wanawake wenye kufahamu huo ni wachache wanaopewa elimu ya kupunguza uchungu wakati wa kujifungua na jinsi ya kudhibiti matatizo ya ujauzito.

Mpango wa hivi karibuni wa watalaamu wa nchini Marekani uliochapishwa na gazeti la The Daily Mail na The Daily Telegraph ulishauri kuongeza nasaha kwa akina mama wajawazito kwa lengo la kuwasaidia kupunguza hofu za uzazi zinazotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa shinikizo la damu (blood pressure) wakati wa kujifungua na hivyo kuongeza hatari ya mwanamke au mtoto kupoteza maisha.

Kliniki nyingi hapa nchini kwa mujibu wa uchunguzi wangu zimekuwa hodari kuwapatia wajawazito majibu yatokanayo na vipimo na kutojali umuhimu wa nasaha, jambo ambalo huwafanya wakina mama wengi kukosa elimu ya kutosha kuwasaidia. Lakini upande wa pili, wajawazito nao wamekuwa wakishindwa kuwasiliana barabara na wakunga kwa lengo la kujifunza juu ya uzazi salama.

Kitalaamu kujua jambo kunaongeza hofu hasa ujuzi huo ukikosa maelekezo ya ziada kuhusu kinga. Kwa mfano ni hatari zaidi kwa mwanamke kusikia tu kwamba wakati wa kujifungua huwa na maumivu makali bila kuambiwa anawezaje kuyapunguza. Katika hali ya kawaida mwili ulioandaliwa kupokea pigo fulani kwa mfano, hujenga hali ya kinga ambayo husaidia kupunguza maumivu.

Hii ina maana kwamba uchungu wa mwanamke aliyeandaliwa kisaikolojia kukabiliana na maumivu wakati wa kujifungua utatofautiana sana na yule ambaye mwili wake hakuandaliwa kushindana na uchungu huo. (Hakikisha hili kwa kujiandaa kupigwa na pigwa ghafla, kisha upime mshtuko na maumivu yake.)
Wanawake wengi wanaokumbwa na matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua kwa mujibu wa uchunguzi uliohusisha majibu ya wakunga katika Hospitali za serikali za jijini Dar es Salaam, Tabora, Kigoma na Mwanza ni wale wa uzazi wa kwanza. Sababu nilizozibaini mimi ni uhaba wa nasaha kama nilivyodokeza.
(Hapa nawaondoa wanaobeba mimba katika umri mdogo.)

Inaelezwa na wataalamu kwamba idadi kubwa ya wanawake wa kundi hilo wamekuwa wakipata aidha kifafa za uzazi au kushindwa kujifungua na hivyo kulazimika kufanyiwa upasuaji ili kuwanusuru na kifo. Matatizo yote haya yanatajwa kutokea nyuma ya shinikizo la damu ambalo nimeeleza habari zake hapo juu kwamba huchangiwa kwa kiasi kikubwa na hofu.
Ukiachana na kundi hilo la uzazi wa kwanza, uchunguzi unaonyesha pia akina mama wanaotoka kwenye familia zenye migogoro ya ndoa, waliotelekezwa baada ya kupewa ujauzito na wasiopendwa na jamaa zao wanaongoza kupata matatizo wakati wa kujifungua. Hii inatoa sura kwamba ujauzito unahitaji zaidi faraja kuliko kitu kingine chochote.

Mtaalamu Joanne Lally kutoka Chuo Kikuu cha Afya ya Jamii cha Newcastle na timu yake waliweza kubainisha mambo mengi ya msingi kuhusu uzazi salama, lakini kubwa kabisa ni faida za kumfariji mzazi mtarajiwa kabla ya wakati wa kujifungua. Kasoro kubwa ya wakunga na walezi wengi wanaohudumia wajawazito ni kuwavunja moyo na kutowajali, jambo ambalo huchangia matatizo wakati wa uzazi.

Nakumbuka nilimuuliza dada Husna (si jina lake halisi) aliyejifungua hivi karibuni mtoto aliyekufa katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, nini kilimpata wakati anajifungua aliniambia hivi: Nilishikwa na uchungu saa saba mchana, wakati huo mume wangu alikuwa kazini. Majirani wakanikimbiza hospitali ya Mwananyamala. Nilifika nikiwa na maumivu makali ambayo sikuwahi kuyapata, nikawa nalia kuomba msaada wa manesi, lakini hawakunijali kabisa.

“Basi nikawa navumilia, uchungu ulipozidi ndo manesi wakaja, wakawa wananiambia sukuma, sukuma kwa nguvu huku wananitukana, kusema kweli nilizidiwa na uchungu mpaka nikapoteza fahamu nilipozinduka wakaniambia nilijifungua mtoto akiwa amefariki, kusema kweli niliumia sana.” Mwisho wa simulizi ya Husna.

Katika hali ya kawaida Husna na wanawake wengi huenda kujifungua huku wakiwa na historia kwamba kuna uchungu mkali wakati wa kujifungua, lakini ni kwa kiwango gani na wanawezaje kuupunguza? Hili ni swali gumu, na bila shaka ni wanawake wachache sana waliofundishwa elimu hii na kujiandaa kupunguza maumivu wakati wa kujifungu.


Namkumbuka muuguzi Stacey Rees wa Brooklyn, New York, katika mada zake juu ya uzazi salama alisema, kitu cha kwanza kabisa kukusaidia wakati wa kujifungua ni utulivu wa akili yako.
Hapa ina maana kwamba kila mjamzito anatakiwa kutafuta na kupewa utulivu ndani ya akili yake. Njia pekee itakayomsaidia ni kujifunza namna ya kupata majibu ya matatizo na wasiwasi wake juu ya ujauzito na kujifungua.

Inashauriwa kwamba kila mjamzito anatakiwa kutafuta mkunga au mshauri wake, atakayemuelimisha kuhusu mimba, kumfumbulia matatizo yake na kumpa ushauri juu ya mabadiliko ya mwili, maumivu, ikiwemo nasaha. Ni wazi kwamba maneno ya kusikia huwaogopesha wajawazito.
“Kama tumbo linakuuma chini ya kitofu inawezekana ukawa na tatizo.” “Unaumia upande gani? Huu, basi mtoto atakuwa amekaa vibaya tumboni.” “Amefariki wakati anajifungua.”
Hizi ni kauli mbaya kwa mjamzito kuzisikia inabidi aondolewe kwa kuambiwa maneno kama haya: “Usiogope, kama maumivu yanatokea mtoto anageuka tu, hata mimi ilikuwa hivyo wakati wa ujauzito wa x.” Aaah, siyo sana ukijitahidi kusukuma wala hutaumia sana.” Nasaha za aina hizi zinajenga sana imani ya mjamzito na kuongeza ujasiri wa kukabiliana na matatizo.

Katika Jarida la American Baby mtaalamu mmoja iliwahi kuandika faida ya mwanamke mjamzito kufanya mazoezi wakati wa ujauzito yenye lengo la kumuwezesha kuwa na pumzi ya kutosha. Wengi kati ya wanawake hupenda zaidi kula na kuwa wavivu kufanya kazi au mazoezi, jambo ambalo huongeza uzito wa mwili na kuathiri mfumo wa upumuaji. Haishauriwi mjamzito kushinda amelala au kukaa, ni vema akamuona madaktari amshauri kuhusu aina ya mazoezi kulingana na umri wa ujauzito wake. (Onyo mwanamke asifanye mazoezi bila ushauri.)
Lakini pia muuguzi Ina May Gaskin, anasema katika maneno yake kwamba kuamini kwamba ujauzito si tatizo ni njia ya kuujengea mwili uwezo wa kukabiliana na maumivu wakati wa kujifungua.Labda swali ni kwamba wanawake wangapi wanaosaidiwa kujiamini wakati wa ujauzito wao? Kipimo cha tatizo hili kinaweza kuwa ni kigumu lakini ikiwa mjamzito anaishi kwa hofu nyingi zitokanazo na matatizo ya kujifungua ni dhahiri hajiamini.

Njia nyingine ya kupunguza maumivu wakati wa kujifungua inatajwa kuwa ni kupenda mtoto atakayezaliwa. Mapenzi haya ya kupata mtoto anaweza kumsaidia mama mjamzito akavumilia na kuyaona maumivu kuwa si kitu zaidi ya kujifungua. Ushahidi wa hili unapatikana kwa wanawake wanaoamua kutoa mimba baada ya kutopenda kuzaa. Kwao maumivu huwa ni kitu kidogo ukilinganisha na nia yao ya kutoa mimba.

Aidha nilidokeza hapo juu umuhimu wa kufanya mazoezi, lakini ukweli ulio wazi umebainika kuwa wanawake wanaotembea tembea wodini au nje kipindi cha kuelekea kujifungua hupata nafuu ya maumivu, kuliko wanaoketi na kulia. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na timu ya wataalamu nchini Marekani ulionyesha wanawake waliotazama picha za wapenzi wao wakati wanaugulia maumivu ya uzazi walitabasamu na kutulia, huku picha za watu waliowachukia zikitajwa kuwaongezea hangaiko.

Jambo kubwa la kukumbuka ni kwamba maumivu na presha ni vitu vinavyokwenda sambamba, hivyo haishauriwi kwa mtu mwenye maumivu kuwa na fikra mbaya, wasiwasi au kuogopeshwa. Nimalizie tu kushauri kwamba mjamzito anatakiwa kuwa karibu na wataalamu wa saikolojia ili kupata msaada wa kukabiliana na hofu ya uzazi ambayo ni hatari zaidi kwa uzazi salama.

Ushauri wa mwisho kama mwanamke anataka kupunguza maumivu wakati wa kujifungua awe hodari kuhudhuria kliniki na aweze kuuliza kila jambo analohisi linamtatizo. Lakini pia ni mwiko wa kitabibu kwa wakunga kuwatia hofu wajawazito kwa kuwaambia maneno ya kukatisha tamaa. Hata kama tatizo lipo mjamzito atiwe moyo wa kwa kuambiwa. “Mtoto amekaa vibaya, lakini ukifanya hivi na vile utajifungua salama tu.”

9 comments:

  1. Asante! Kwa makala Yako nimepata elimu.

    ReplyDelete
  2. Makala nzuri sana. Inapasa kila mjamzito na muuguzi kuyafahamu haya.

    ReplyDelete
  3. Asante sana kwa ushauli wako umenifaliji nakunipa nguvu

    ReplyDelete
  4. Ahsante sana kwa makala nzuriiii na Mungu akubariki sana.

    ReplyDelete
  5. Hakika Nimejifunza kitu! nitamsaidia mke wangu pamoja na wengine pia ili kulinda usalama wa mama na mtoto.

    ReplyDelete