JESHI la polisi hivi karibuni lilisambaratisha maandamano
ya wananafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kwa mabomu, silaha za moto na matumizi
ya nguvu kupita kiasi.
Kwa sababu ya amani ya nchi yangu siungi mkono machafuko,
migomo na maandamano, jambo linalonifanya nisikemee moja kwa moja hatua
iliyochukuliwa na polisi.
Pamoja na uzalendo huo, kasumba ya mkuki kwa nguruwe kwa
binadamu mchungu inanikera sana, sana, sana! Sina mbadala wa kauli hii hata kama
asiyeiabudu falsafa hii ni baba yangu mzazi.
Binafsi niliyashuhudia matumizi ya nguvu ya polisi katika
kukabiliana na maandamamo hayo. Nasikitika kusema hata damu za wanafunzi
niliona zikimwagika. Nikajiuliza chanzo cha tatizo ni nini? Mwanafunzi mmoja
aliniambia:
“Tulipanga kwenda ofisi ya waziri mkuu kuonana naye ili
tuwasilishe madai yetu, tumekuwepo chuoni kama watu tuliotelekezwa, hatuna
chakula na fedha tulizoahidiwa kupewa hatujapewa, fedha za malazi na viandikwa
nazo hakuna, sasa uwepo wetu shuleni una maana gani?”
Hii ndiyo hoja ya msingi iliyoandaa mgomo. Nyongeza ya
madai ya kuongezewa posho ya chakula ilijumlishwa kwenye ajenda katika hali ya
kufikisha hisia zinazowakwaza wanafunzi hao wa programu maalumu iliyoandaliwa
na serikali kwa lengo la kuzalisha walimu.
Upembuzi; ni nani kati ya rais, waziri mkuu, waziri wa
fedha na watendaji wa serikali, mwenye uwezo wa kufanya kazi bila kula? Shujaa
gani anayeweza kutumika kwa moyo bila kuwa na mahali pa kulala na vitendea
kazi?
Jibu hakuna; jambo ambalo linayafanya madai ya wanafunzi
hao kuwa ya msingi yasiyoweza kumalizwa kwa majibu dhaifu ya: “Muwe wavumilivu.”
Mkuu wa idara anayesema wanafunzi
wavumilie njaa yeye tumbo limejaa nyama choma na mvinyo!
Anayehimiza wenzake wavumilie hawezi kutembea kwa miguu
hata hatua kumi. Anayehimiza uvumilivu hajawahi hata siku moja kulala njaa na
isitoshe hajacheleweshewa malipo ya posho zake akavumilia lau kwa mwezi mmoja!
Hili ndilo jambo linalonisikitisha; serikali inawezaje
kutumia nguvu kuwapiga mabomu na risasi watu ambao imeshindwa kuwatimizia ahadi
zao?
Hoja ingejengwa kwamba, wanafunzi hawa wamelipwa kiasi
fulani lakini bado wamekomaa kudai anasa zaidi, watu wangeelewa. Lakini kutumia
silaha za moto kumwaga damu huku udhaifu ukiisuta serikali, haliwezi kuwa jambo
linaloweza kuvumiliwa.
Nimesema mara nyingi, rais anaweza asiwe dhaifu, chama
tawala kinaweza kisiwe cha mafisadi kama watu wanavyodai lakini baadhi ya
watendaji wake hawawezi kukwepa lawama hizi! Na hawa ndiyo kansa ya ustawi wa
jamii.
Nathibitisha; miaka miwili iliyopita baadhi ya watendaji
wa bodi ya mikopo waliingia matatani baada ya kubainika kulipa mikopo hewa kwa
wanafunzi. Mchezo huu siyo mgeni, kwa mpenda haki anaposikia fedha fulani za
mkopo zimechelewa lazima ahoji mantiki yake. Maana siku hizi inadaiwa fedha
hucheleweshwa wakati mwingine kwa sababu zinachezewa upatu.
Kibaya zaidi mamlaka za serikali zimekuwa kimya mno,
ingekuwa sawa basi baada ya malalamiko ya wanafunzi juu ya maisha magumu chuoni,
kutolewe ufafanuzi wa kina na pengine wanafunzi kwa kushirikiana na wakuu wa
vyuo kukutana kutafuta suluhu ya uhakika ili maisha yaende.
Yote hayo hayafanyiki; badala yake serikali inasubiri
watu wagome iamuru wapigwe risasi za miguu, huu siyo utawala bora hata kidogo.
Kinachoniumiza zaidi ni kwamba uhusiano baina ya serikali
na wananchi unaharibika siku hadi siku hivyo kuifanya nchi kuwa katika hatari
ya kuingia kwenye machafuko. Nachochea hivi; serikali inayopiga mabomu raia wadai haki,
yenyewe itapigwa na nini? Akili kichwani!
No comments:
Post a Comment