ENZI za mkoloni ambazo Mkuu wa Kaya nilikuwepo; mpango mahususi
ulikuwa elimu bora ni kwa watu weupe.
Weusi hawapekuwa nafasi kwenye shule bora kwa kuwa mkakati
uliwataka waendelee kuwa mbumbumbu ili wawe watumwa katika mashamba ya mkonge
na katani.
Shukrani ukombozi ukaja, Rais wa Tanganyika Huru, Julius
Nyerere akafuta kikwazo hicho. Mwaka 1964 ukaanzishwa mpango wa elimu bora kwa
wote, lengo likiwa ni kuwaelimisha wazawa wapate uwezo wa kujitawala.
Kwa kiasi fulani hilo lilifanikiwa. Wakati mwingine
nikiwasikia hawa wazeewazee wanaojifanya wajuaji kwenye kaya yangu huwa
nawaangalia halafu nacheeeeeka, kwa
sababu najua wao hawakutengwa katika elimu enzi za utoto na ujana wao lakini
bila aibu siku hizi kwa kupewa vivyeo uchwara wanawasahau watoto wa wakulima.
Leo ukienda shule za kata humkuti mtoto wa mkuu wa mkoa wala
wa katibu tawala, wote wanasoma shule za akademi zinazofundisha kwa kimombo.
Ukiwahoji kulikoni ninyi viongozi mjitengenezee ka-utaratibu ka-ubaguzi? Wanakujibu,
shule za kata hazitoi elimu bora, ujinga kabisa! Kama hazitoi elimu bora uongozi wao kwenye kaya
hii una faida gani? Hasiraaa!!
Hivi mwenzao naye (Nyerere) angefanya kama wanavyofanya nchi
hii, wao si wangekuwa walima nyanya tu? Kwani alikuwa na shida gani kuwasaidia
wapate elimu bora wakati leo wanashindwa hata kumuenzi!
Lakini kwa kuwa aliwaza ukombozi, alifikiri zaidi ya familia
yake, alikuwa muumini wa mafanikio ya wengine alianzisha elimu bora kwa wote;
matokeo ambayo yameleta matunda ya watu wasomi wengi wanaolisaidia taifa kwa
namna fulani kipindi hiki.
Swali; ninyi viongozi mnashindwa nini kuifanya elimu ya nchi
hii kuwa bora kwa kila mtu? Ukiangalia takwimu za ufaulu wa darasa la saba
mwaka huu utangundua kuwa karibu nusu ya wanafunzi tena wenye umri mdogo
wamefeli, ukimuuliza waziri mwenye dhamana; hao wanafunzi waliofeli anawapeleka
wapi kupata elimu maana siyo ombi ni haki yao ya kikatiba, ‘atachekacheka’ tu!
Ukimuuliza wanafunzi wa kidato cha nne waliofeli mwaka jana serikali
yake chini ya wizara yake imewaandalia mazingira gani ya kujielimisha,
imewawekea mkakati gani wa kuondokana na ukosefu wa ajira, amewapangia utaratibu
upi wa kujielimisha ili waendane na kasi ya ulimwengu wa sayansi na teknolojia?
Huwezi kupata jibu la uhakika ni kuchekacheka tu.
Wakoloni hawakupenda
kuwasomesha wazawa kwa sababu walitaka watumwa wa kuwafanyisha kazi ngumu. Je,
huu mpango wa serikali wa kutowajali wanafunzi zaidi ya nusu wanaofeli kila
mwaka umejikita katika kujiandalia mahausigeli na mahausiboi katika nyumba za
viongozi na mashamba ya watoto wa wakubwa wa nchi hii?
Kama sivyo kwa nini hakuna mipango thabiti ya kuwapatia
elimu? Ukiiangalia elimu ya leo imejaa upendeleo kila mahali; inawezekanaje
wanafunzi wanaosoma vijijini kusikokuwa na maabara, umeme, wala shule za awali
wakashindanishwa mtihani mmoja na wanafunzi wanaosoma shule za akademi?
Mimi kama Mkuu wa Kaya naziona kasoro hizi katika kaya yangu
na wananzengo wenzangu kwa nini mawaziri wanaolipwa mishahara na marupurupu
makubwa akili zao haziwafikishi kwenye kiwango hiki cha utambuzi?
Naona kwa utaratibu huu wa kutowasaidia wanaofeli zaidi ya
nusu kwa miaka 20 ijayo taifa litakuwa na mbumbumbu zaidi ya nusu ambao
hawatakuwa na sifa ya kuendana na kasi ya ulimwengu wa sayansi na hivyo
kulirudisha taifa hili katika utumwa wa fikra alioupinga Nyerere.
Hivi inashindikana nini kujipanga kuhakikisha kuwa elimu
katika kaya yetu inakuwa bora kwa kila Mtanzania? Tuliwachoka wakoloni
tukawaondoa madarakani bila shaka tutawachoka watawala wavivu wa kufikiri na
kuwaondoa.
No comments:
Post a Comment