Thursday, January 22, 2015

Jambo gani ni muhumu; kupenda au kupedwa?



UCHUNGUZI unaonesha kuwa, watu wengi waliopata kuulizwa swali lililopo kwenye kichwa cha makala haya walipendelea zaidi kupendwa.
Ni nadra sana mtu kujinung’unikia juu  ya udhaifu wa kutopenda, kuliko lawama za kuwalaumu wengine kuwa hawampendi.

Je hivi ndivyo mambo yanavyotakiwa kuwa? Jibu ni hapana; kwani sayansi ya ufahamu na nafsi haielekezi hivyo kwa sababu upendo ni sawa na mbawa za ndege ambazo huwezi kusema bawa la kushoto ni muhimu kuliko la kulia.
Chunguza kwa kujiweka kwenye fungu la mtu wa kupendwa usiyekuwa na chembe hata ya upendo kwa wenzako.
Jaribu kuufungua moyo wako upokee mapenzi ya wengine tu bila kurejesha chochote kwao. Kisha angalia furaha ya moyo wako, bila shaka upendo hautakukidhi, utajiona uko kwenye upungufu fulani.
Ukiachana na hilo weka maisha yako kwenye kupenda tu na usirejeshewe mapenzi ya wenzako, hapo napo utabaini kuwa moyo wako una ganzi na uhitaji wa furaha timilifu; naamini lipo jambo la kukubaliana kwenye mambo haya mawili.
Ikiwa hivi ndivyo, tujiulize inakuwaje watu wengi huwa wanatamani kupendwa? Jibu rahisi ni kuwa, wengi hukwepa gharama za kupenda.
Maana katika hali ya kawaida kupenda huambatana na gharama na wakati mwingine kukubali kuwa mtumwa wa mtu fulani, kujitoa kwa ajili ya kutimiza upendo kwa wengine.
Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa, wachagua kupedwa kwa msukumo wa kukwepa gharama hawajawahi kujitoa kwenye ukweli wa upendo kuwa sawa na mbawa za ndege kwani hata wakiacha kupenda bado wanagharimika.
Ni wazi; kumvutia mtu akupende nako kuna shida zake na kibaya zaidi utumwa utegemezi wa akili na mahitaji ni gharama inayotajwa kuwa kubwa na mbaya zaidi.
Umewahi kujiuliza mateso ambayo huyapata wanaopendwa pale wanapobaini kuwa waliowapenda wamewaacha.
Kwa kuwa siyo msingi wa mada hii kuelezea hayo; ni bora kurejea kwenye msingi wa somo letu kwa kuweka wazi jambo moja kuwa, upendo ni mbegu inayoota na kuzaa matunda ya jinsi yake.
Ukitaka kuyafanya maisha yako yawe mazuri, yatoe mafanikio mengi, basi ifanye mbegu ya upendo aliyoipanda mumeo/ mkeo, ndugu jamaa na rafiki zako izae moyoni mwako.
Usiishie kutafuta wa kukupenda jaribu kutafuta wa kumpenda pia hata kama utaniuliza swali zoefu kuwa wengine hata hawapendeki; hicho usikifanye kuwa kikwazo cha maisha yako ya furaha kwa sababu hujui unayeishi naye ameletwa duniani kufanya nini na lini ataondoka.
Kwa kumalizia makala haya hebu yaweke maisha yako kwenye kipimo. Ni mara ngapi umejisifia mbele za wenzako kuwa unapendwa? Je upendo huo umekuwa na maana kwenye maisha yako?
Mtafakari mpenzi wako, muunganishe na hisia zako kisha ujipime amekuletea furaha toshelevu? Ikiwa moyo wako unaona bado haujatosheka naye tambua kuwa hujalipa upendo wake na kwamba unajitesa moyoni na kuuongopea ulimwengu kuwa unapendwa.
Baada ya kutazama hilo, jaribu kugeuza upande mwingine  kwa kujiuliza upendo wako umekuletea furaha timilifu. Unalidhika kumpenda mtoto wako kiasi cha kusikia furaha isiyo na kifani? Kama kuna dosari hufiki kwenye kilele tambua unaudanganya ulimwengu. Upendo wa kweli haupo!
Kwa leo naomba niishie hapa wakati mwingine nitachambua zaidi somo hili kwa kuangalia misingi ya upendo na kuelezea aina zake kwa undani zaidi. Asante kwa kuwa nami karibu tena Alhamisi ijayo kwenye mada nyingine nzuri zaidi!

No comments:

Post a Comment