Watu wengi huhangaika sana kujua kama wanaifurahisha
jamii au wanaiudhi. Wengine wamefikia hatua ya kujiuliza, wamekosea nini watu
wanaowazunguka mpaka wakajikuta
wamechukiwa? Kisaikolojia fikra za namna
hii, ni sawa na kutafuta gari kwenye
mwanga kwa njia ya kupapasa!
“Nashanga mama mdogo ananichukia bure, tena hakuna kosa nililomfanyia lakini
hanipendi tu” Je wewe nawe umekuwa miongoni mwa watu wanaodhani unachukiwa
bure?
Achana na hulka hiyo, hebu tambua ubaya wako kwa
kuangalia vidokezo vifuatavyo, ambavyo naamini ukivisoma kwa umakini utagundua
ni wapi unakosea hadi kufikia hatua ya kuchukiwa katika jamii.
Je, inapotokea umesababisha wenzako wajisikie vibaya huwa
unajisikiaje moyoni mwako? Mfano ulikuwa katika mazungumzo ya kawaida na rafiki
yako, lakini kwa sababu za kibinadamu akapokea mazungumzo yako vibaya na
kufadhaika. Wewe unapotambua kuwa umemuondolea mwenzako furaha huwa
unajisikiaje moyoni? Kama huumizwi na tukio hilo tambua kuwa wewe ni mtu mbaya.
Jiulize, katika maisha yako ni mara ngapi umewafanya
wengine wafurahi kwa kuwatatulia matatizo yao, kuwasaidia katika shida na
kuwavusha katika hali ngumu za kimaisha? Au umekuwa mtu wa kusubiri usaidiwe
wewe hata kwa vitu unavyoweza kuwasaidia wenzako?
Tangu umeanza kazi umeshawahi kutoa sehemu ya mshahara/pato
lako kuwasaidia wazazi na ndugu zako au umekuwa mtu wa kutoa visingizio vya
hali ngumu ya maisha licha ya kuwa unafanya anasa mjini? Ikiwa hujawahi
kuwasaidia watu kupata furaha, fahamu kuwa unaishi na ubaya kwenye jamii, jiandae kuchukiwa.
Je, unaposikia wenzako wana shida huwa unazichukuliaje?,
je ni sehemu ya tatizo lako au hujiweka pembeni na kuwaachia binadamu wenzako
wamalize matatizo yao? Ukiwa hivyo hicho ni kipimo kikubwa cha ubaya wako kwenye
jamii unayoishi.
Umekuwa ukitumiaje uwezo wako wa mali au hata nguvu za mwili mbele ya
wenzako? Je, ni kwa kuonea na kuwakandamiza watu uliowazidi? Ikiwa una tabia hiyo anza
kujihesabu kuanzia leo kwamba wewe ni mtu mbaya mbele ya jamii.
Angalia mazungumzo yako, je yamekuwa ni ya kuwatia moyo
watu, kuwafariji na kuwaelimisha au umekuwa mtu wa kutoa matamshi ya
kudhalilisha, kuudhi na kuwavunjia heshima wenzako? Kama ulimi wako unatoa
maneno yenye ‘sumu’ usitegemee kupendwa.
Je umekuwa mtu wa haki, mwenye kuwatanguliza wenzako?
Unaweza kutoa unachokitegemea ili kumsaidia binadamu mwenzio? Ukiwa huwezi
kufanya hivyo na umekuwa mtu wa kukumbatia mali zako ujue wewe ni mbaya.
Toka ndani ya moyo wako unafurahia jamii kuwa na umoja au
umekuwa mtu unayechochea migawanyiko baina ya watu wanaopendana? Endapo una
tabia kama hiyo fahamu kuwa matendo yako ni mabaya.
Ni mara ngapi umezuia hasira zako kwa lengo la kuepusha
migogoro? Unaweza kuvumilia kuonewa au umekuwa mtu wa kulipa kisasi kwa
kudhamilia kufanya mambo mabaya kwa makusudi licha ya moyo wako kukuonya mara
nyingi usifanye hivyo? Kama una tabia hiyo tambua kuwa huo ndiyo ubaya wako
kwenye jamii, chukua hatua za kujisahihisha wewe kwanza kabla ya kuwanyooshea
wenzako kidole!
No comments:
Post a Comment