Ni watu
wachache ambao wanaweza kujisifu kwa uhodari wa kutafuta. Naamini ni nadra
kumkuta mtu akifurahia kubeba mzigo mzito, kulima, kufanya kazi, kujituma
katika shughuli hii na ile kwa sababu kutafuta tunakuchukulia kama kero.
Ni rahisi
kutamani kufanya kazi kidogo lakini si kupewa fedha au mgao wa mafanikio kwa
kiwango kidogo. Tamaa ya wanadamu wengi ni kupata na si kutafuta.
Kwa msingi
huo, sioni haja ya kusubiri jibu la kipi bora kati ya kupata na kutafuta kwa sababu
najua; vijana wengi wanatamani sana kupata kazi nzuri, kuwa na fedha nyingi za
kufanyia anasa, mavazi ya gharama na nyumba
za kisasa. Hivyo chaguo lao ni kupata.
Kitalaamu,
miongoni mwa makosa makubwa yanayofanywa na watu ni kupenda kupata na kuchukia
kutafuta. Msomaji wangu, utajiri si wingi wa pesa au mafanikio bali kufanya kazi
na shughuli nyingi zaidi ya mafanikio uliyopata.
Siku zote wanaofanikiwa
duniani ni wale wanaopenda kutafuta, hawachoki kuwekeza, hawaachi kujitumikisha,
hawatafsiri faida kama pato la kutumia kwa anasa bali nyenzo ya kuwawezesha kutafuta
zaidi.
Mchanganuo
wa mambo haya mawili uko hivi: KUPATA; mfumo wake ni matumizi. Mtu aliyepata
mshahara akafurahi, akalidhika, hana njia nyingine zaidi ya kuutumia mshahara
huo kununulia nguo, kulipia umeme, pango la chumba na ada za shule.
Ukweli ni
kwamba, hata kama fedha na mafanikio aliyopata mtu yatakuwa makubwa kiasi gani
kwa mfumo huu wa kutoa, matokeo tarajiwa ya siku za usoni ni kumalizika kwa
pato na hivyo kumpeleka mtu kwenye hatua ya nyingine ya kutafuta.
Lakini KUTAFUTA;
ni mrija uvutao mafanikio. Nayetafuta hupata zaidi na zaidi na uzuri wake ni
kwamba, mfumo huu umeunganishwa moja kwa moja na KUPATA. Kwa msingi huo
anayetafuta anakuwa sawa na mtu anayeishi ndani ya mifumo miwili kwa mpigo na
kwake mtu huyo hakuna kufilisiki bali apataye hufilisika.
Nashauri,
watu wote tufurahi zaidi wakati wa kutafuta, tujivunie uwezo wa kutenda,
tupende kazi zinazotuingizia mishahara na kamwe tusipende mishahara
inayotupeleka kwenye matumizi yatakayoturudisha kwenye mfumo wa kutafuta
tusioupenda.
Muhimu
kuunganisha nguvu katika harakati za kutafuta maisha na kuachana na mfumo wa
kushirikiana zaidi kwenye matumizi ya vile tunavyopata kwa sababu mwisho wake
ni mbaya.
Nimalizie
makala haya kwa kuwashukuru wasomaji wangu wote kwa kuniunga mkono katika safu
hii, siku zote nafurahi kusikia jinsi ambavyo makala zangu zimekuwa
zikibadilisha maisha ya watu.
Kazi nzuri. Keep it up :)
ReplyDeletesawasawa
ReplyDelete