HAKUNA kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika
daraja la chini na mtu wa kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia
kuna madhara makubwa.
Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa
lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu
jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Kitaalamu, hakuna jambo ambalo hutokea maishani bila sababu
maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako au kwetu ndani ya jamii tunayoishi kunatokana
na jinsi tunavyoenenda.
Mwalimu wangu wa somo la maisha na saikolojia, Eric
Shigongo, aliwahi kuniambia ‘Nothing happens in the sky, but the elements
should be there,’ akimaanisha kuwa
hakuna kitokeacho angani pasipo kuwa na dalili au sababu zake.
Naomba nianze kutoa njia za kukusaidia kurejesha heshima
yako kwa kuperuzi na wewe baadhi ya dokezo muhimu zinazoweza kukusaidia kujitambua
na kuweza kuyaepuka maisha ya kudharauliwa.
MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi unavyoonekana. Muonekano
ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku moja
hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana kipaji
kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili huchangia mtu
kudharauliwa katika jamii anayoishi. Linaweza kuwa jambo dogo sana lakini ni
moja kati ya sababu kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani yako mbele ya
wenzako.
Mazungumzo
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza
kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara zitakufanya
udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha
heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi. Biblia inasema penye wingi wa
maneno hapakosi uovu.
UTENDAKAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi
kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza kwa tabia ya kuombaomba,
jambo hilo halifai kwa vile huchangia kubomoa heshima yako mbele ya jamii.
Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.
KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa
kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza heshima yako katika
jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na kutotimiza.
SIFA ZISIZO NA
MAANA
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa mwandishi mwandamizi
aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha, marehemu Adolf Balingilaki, ambao
unasema kwamba:
“Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau
kwa bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo
yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu watakudharau.
KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri,
dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze
kwani ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.
No comments:
Post a Comment