Imani
iliyojengeka kwa wengi katika jamii yetu ni kuwa, ushauri ni kitu muhimu sana
kwa kila hatua.
Kwa mtazamo wa harakaharaka
unaweza kuishia kwenye ukomo huo wa fikra na kuamini juu ya ushauri wa mtu
kukufikisha mahali sahihi kwenye maisha. Unapokwama kimaisha unakimbilia
kushauriwa, wakati mwingine hata unapotaka kuoa au kuachana na umpendaye,
unamuomba rafiki yako ushauri.
Je, umeshawahi kufikiria
hasara za kuomba ushauri wa kimaisha kwa rafiki yako? Hebu ungana nami
nikumegee kidogo hasara za ushauri.
UTAKUPOTOSHA
Ni wazi kwamba kipimo cha
uelewa kinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Ifahamike kuwa,
uhodari wa mambo nao hutofautiana, mtu anaweza kuwa mahiri katika siasa na
akaaminika kwenye jamii, lakini ukimpelekea suala la mapenzi anakuwa hajui
kitu, hivyo ni rahisi kukupotosha.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, watu wengi sana
hupotoshwa na rafiki zao wasiokuwa na uelewa wa kutosha juu ya tatizo au suala
husika la kimaisha. Ushauri wangu ni kuwa makini kila unaposhauriwa.
UTARAHISISHA MAMBO
Mara nyingi washauri huwa si
wao wanaokabiliana na mambo, hivyo ni rahisi kwao kupima vitu kwa juujuu tu na
kushauri kirahisirahisi.
Ni rahisi kumsikia mshauri
akisema: “Vipi kakupiga namna hii, aaa huyu si mwanaume kwa kweli ni bora
ukaachana naye.”
Anasema ni bora kuachana naye
kwa sababu haumizwi na kuachana, unayeachana ni wewe anayekushauri.
“Tatizo hili ni dogo sana,
kama hataki kukulipa mpeleke mahakamani.” Kwa mshauri ni rahisi kusema hivyo
lakini kumbuka ukubwa wa usumbufu wa kwenda mahakamani kupoteza muda litakuwa
ni suala lako si lake tena. Uwe makini na ushauri unaorahisisha mambo.
UTAKUGEUZA
Ulimwenguni kuna watu wa kila
namna wenye mapenzi na mguso tofauti wa kimaisha, hii inamaana kwamba mtu
fulani hawezi kulingana na mwingine kwa kila kitu; ni nadra sana.
Uzoefu unaonyesha kuwa,
washauri wengi hushauri kwa uzoefu wao na mapenzi yao, lakini je ni sahihi
uzoefu na mtazamo wao uwe msaada kwa watu
wengine?
Jibu ni hapana, kinachotokea
mara nyingi kwenye ushauri ni mtu kumfanya mwenzake awe kama yeye alivyo, yaani
apuuze, aamue na apende kama staili yake, jambo ambalo haliwezekani kabisa.
Vipi Juma ageuke ghafla awe kama Hassan kwenye suala la mapenzi? Ushauri ni
muhimu lakini upime kama unalingana na matakwa yako.
UTAKUONDOLEA UJASIRI
“Kwa maelezo hayo mumeo ni
malaya sana, naona itakuwa vigumu kumbadilisha, ni bora ukaanza maisha yako kwa
sababu kuna siku hali itakuwa mbaya.”
Huu ni ushauri ambao unaweza
kumuondolea mtu ujasiri wa kukabiliana na tabia ya mumewe hadi kufikia hatua ya
kumsaidia akaachana na tabia zake mbaya.
Ushauri huondoa ujasiri wa kukabili
tatizo hasa pale anayekushauri atakapolipeleka suala lako kwenye njia ngumu
isiyokuwa na ufumbuzi. Ikumbukwe kuwa anayeamini kushindwa ni mshauri lakini
wewe kama binadamu mwenye uwezo mkubwa unaweza kusimama kutetea penzi lako na
kuliweka sawa mpaka jamii ikasema: “Jamani huyu dada kamrekebisha kweli mumewe,
hakuwa hivi alikuwa mlevi lakini sasa kaacha pombe.”
UTAKUNYIMA FURSA
Kwenye maisha kuna fursa
nyingi za mafanikio ambazo unaweza usizipate ukiwa mtu wa kusikiliza sana
ushauri wa watu. Kuna wakati ambao unatakiwa usimame wewe kuamua ufanye nini
hata kama jamii na washauri watakuona kama unakosea. Akili za kuambiwa
changanya na zako, wanasema waswahili.
No comments:
Post a Comment