NI imani yangu kuwa, si wote wanaofahamu kwamba duniani
kuna makundi manne ya watu wanaotafuta mafanikio, jambo linalochangia kwa kiasi
kikubwa kuwafanya wakose majibu ya kwa nini hawa wafanikiwe kimaisha na wengine
wasifanikiwe kabisa.
Kwa kufahamu hilo, nimeona ni vyema nikaandika makala
haya kuhusu aina za watu katika ulimwengu wa mafanikio ili kuamsha akili za
watu katika kukabiliana na changamoto nyingi za kimaisha.
Katika ulimwengu wa mafanikio binadamu wamegawanyika
katika makundi manne ambayo ni WATENDA USAHIHI, WANAOLIDHIKA, WANAOTAKA
KUPENDWA NA WASHINDI.
WATENDA USAHIHI:
Ni watu ambao katika maisha yao huwa
hawataki kukosea au kuonekana wayafanyayo si sahihi. Watu wa aina hii huwa ni
wagumu sana kufanya jambo ambalo akili zao hazihakiki kuwa litamalizika kwa
mafanikio.
Kikwazo kikubwa kwa watu wa aina hii mara nyingi ni kusitasita
katika kuamuzi. Ni watu wa kuogopa macho ya watu hasa suala la kushindwa
kutimiza malengo linapowajia akilini. Kinachowaogopesha zaidi watu wa kundi
hili ni kuaibika mbele za watu jambo fulani likiwaharibikia.
WANAOLIDHIKA:
Kundi jingine la watu katika ulimwengu wa
mafanikio ni wale wanaolidhishwa na hali zao na kwamba hawahitaji mabadiliko ya
aina yoyote kwenye maisha yao.
“Ndugu yangu, hali hii tumeizoea, mwaka wa nne
huu.” Wamezoea maisha magumu na hawataki kujituma kutafuta.
Hata hivyo, wapo wanaozoea kazi na majukumu yao ya kila
siku kiasi kwamba hawataki kubadilika, hawapendi kuongezeka zaidi ya hapo
walipo. Utakuta uwezo wa mfanyakazi alioanza nao miaka 7 iliyopita ni huohuo
mpaka leo.
Wafanyakazi wengine wanaweza kuajiriliwa nyuma yake
wakajitahidi kusoma, kujifunza kazi na kupanda vyeo na kumwacha mlidhikaji yuko
palepale. Kundi la wanaolidhika.
WANAOTAKA KUPENDWA:
Kuna watu katika maisha yao wanataka
kumfurahisha kila mtu kwa lengo la kuvuta upendo wa wanadamu wenzao.
Asilimia kubwa ya kipato chao hukitumia kwa lengo la
kuwatumikia ndugu na marafiki, kuwasaidia katika shida zao na kujikuta
wakisahau kufanya mambo yao ya kimaendeleo.
WASHINDI:
Kundi la mwisho la watu ni wale ambao katika
maisha yao ya kila siku hupenda kufika kwenye kilele cha mambo yote
wanayofanya.
Hutamani kufanikiwa zaidi na zaidi, hawakubali jambo
liwashinde, kila walichokusudia kukifanya huakikisha kwamba wanakabiliana na
changamoto zote na mwisho wa safari kupata ushindi.
Baada ya kuangalia hayo, ni vema kujiuliza; Je ni sahihi
kutokuwa makini katika mambo yako ama kulidhika na mafanikio uliyoyapata? Je ni
sahihi mtu kuacha kuwasadia wenzake kwa hofu ya kuwa katika kundi la tatu?
Jibu ni hili: Ni vema mambo matatu ya mwanzo yakaongozwa na la nne yaani
USHINDI. Kwa maana hiyo kila mmoja wetu lazima awe mtu ambaye anatamani sana
kufanikiwa katika maisha yake ya kila siku.
Watu wote wakiwa na nia hii wataweza kuyapita makundi mengine matatu kwa
uangalizi mkubwa.
Hawatakubali wawe makini wasifikie malengo, hawataacha
kujaribu bahati kwenye mambo ambayo akili zinaona ni magumu, hawatalidhishwa na
mafanikio au hali walizonazo na hawatakubali kutumika kama wafurahisha watu
bali kwa kila kitu watafanya kwa kiasi kwa lengo la kufika katika mafanikio
sahihi.
No comments:
Post a Comment