Wednesday, April 16, 2014

Jinsi ya kuanza maisha ya kujitegemeaUCHUNGUZI unaonesha kuwa kila mtu anapenda kujitegemea, lakini wengi wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya kukosa kitu wanachokiamini, nacho ni kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo!
“Napenda sana kujitegemea lakini sina uwezo,” wengi hutamka hivyo unapowauliza kwa nini wanazeekea kwenye maisha ya utegemezi. Sababu ya kukosa uwezo imewafanya baadhi ya watu kuwa tayari kupokea kila aina ya manyanyaso na mwisho wa yote wanajipoza kwa kulia.

Swali la kujiuliza:  Ni nani aliyezaliwa anajitegemea? Jibu ni hakuna, hapa ndipo penye msingi wa mada hii ambayo naamini kupitia vipengele vifuatavyo msomaji wangu utajifunza jinsi ya kuanza maisha ya kujitegemea.

MTAZAMO
Kikwazo cha kwanza kinachowafanya watu waishi maisha ya utegemezi ni mtazamo.  Wengi wanaamini wana haki ya kulelewa na wazazi/ndugu, lakini wanashindwa kujiuliza wataishi katika utegemezi mpaka lini na wanaowategemea wakifariki dunia wataishije?
Kazi ya kwanza katika kuyaelekea maisha ya kujitegemea ni kubadili mtazamo wa maisha tegemezi na kuona umuhimu wa kujitegemea.  Maana yangu hapa ni kuyachukia maisha ya kumtegemea mtu na kutamani maisha ya kujitegemea ambayo ni huru na yenye raha.

KUJITEGEMEA NDANI YA UTEGEMEZI
Baada ya kubadilisha mtazamo, mhusika ni lazima aanze maisha ya kujitegemea ndani ya utegemezi. Msingi wa kipengele hiki ni huu; kuna baadhi ya watu wanabweteka mno na kutaka wafanyiwe kila kitu na walezi wao ambapo hata andazi la shilingi 100 wanataka wanunuliwe! Kisingingizio ni kilekile, kwamba hawana uwezo ingawa fedha kama shilingi mia mbili wanazipata.
Kujifunza kujitegemea lazima kuanzie ndani ya maisha ya kutegemea, mfano kama jukumu la baba ni kununua mboga na wewe umebahatika kupata kiasi cha fedha kwa njia yoyote hata ya kupewa, usizifiche, badala yake lichukue jukumu la baba na kulifanya wewe.  Tabia hii inajenga msingi wa uwajibikaji ambao ndiyo nguzo ya maisha ya kujitegemea.
Chukia maisha ya kufanyiwa kila kitu, jihangaishe kwa kazi ya aina yoyote, jiwekee utaratibu wa kuhudumia familia yako, weka msingi wa kuheshimu fedha, usiendekeze tabia ya kupata fedha na kuacha kufanya jambo la maana nyumbani kisa unamtegemea mtu atakununulia hiki na kile na kuzifanya fedha zako ziwe za kutapanya ovyo. Ukijizoeza hivyo hutaweza kujitegemea.
Kwa leo naomba niishie hapa, ila nikuache na swali hili: 

Ni mara ngapi umekuwa ukimsaidia mlezi wako kukabiliana na changamoto za kuendesha maisha?  Kama unafanya hivyo tambua umeanza mazoezi ya kujitegemea, endelea kufanya hivyo lakini kama umebweteka tu nyumbani tambua uzee utakukuta ukiwa mtumwa wa mtu. 


KUJIAMINI
 Vikwazo au shaka juu ya kuweza kumudu maisha ya kujitegemea vimewafanya wengi wasijiamini. “Kwa kipato hiki nitaweza kweli kuendesha maisha yangu, nilipe kodi ya nyumba, chakula, mavazi na mahitaji mengine?” Maswali ya aina hii mara nyingi yamekuwa na majibu ya haitawezekana!

Tabia ya akili hasa katika kufikiria mambo yajayo ni kujenga hofu ambayo wakati mwingine haihitajiki; wenye kujiamini pekee ndiyo ambao hutupilia mbali hofu na kujiamini ndiyo walioofanikiwa katika maisha yao.
Kwa msingi huo, unapofikiria maisha ya kujitegemea usiwaze sana juu ya kuwezekana kwa mambo, jiamini kuwa utaweza, ukifanya hivyo utaweza; siku zote mwenye shaka havuki mto!

KUCHUKUA HATUA
Hatua nyingine muhimu baada ya kupita vipengele nilivyoanisha hapo juu ni hiki cha kuchukua hatua. Watu wengi wamekuwa wakipanga kujitegeme, lakini kila mwaka wanaahilisha kufanya hivyo. “Nafikiri nitahama mwaka ujao.” Mwaka ukifika anapanga kufanya hivyo mwaka unaofuata matokeo yake anazeeka akiwa kwenye maisha tegemezi.

Ushauri wangu, baada ya kujiamini kuwa unaweza chukua hatua ya kutoka mahali ulipo, jambo kubwa la kuzingatia hapa ni kuhakikisha kuwa uchukuaji hatua lazima uambatane na ushauri mzuri kutoka kwa ndugu na jamaa na hasa wale uliokuwa unaishi nao kama wanakuunga mkono katika suala hilo.

KUTORUDI NYUMA
Uchunguzi unaonesha kuwa wapo watu ambao hupitia hatua zote za kuelekea kujitegemea, lakini wanapozikabili changamoto za maisha hayo huamua kurudi mahali wapokuwa wanaishi jambo ambalo huwaongezea fedheha na mara nyingine kuwaathiri kisaikolojia.

Unapokuwa umeanza maisha ya kujitegemea suala la kurudi ulipotoka lisiwe la kawaida. Kumbuka unapokuwa na wazo la “nikishindwa narudi kwa baba,” huwezi kujituma, hutapambana na changamoto za maisha binafsi kwa vile kinga yako haitakuwa kwako bali kule ulikotoka, kushindwa itakuwa ni sehemu yako.

ONGEZA MARAFIKI
Unapokuwa kwenye maisha ya kujitegemea hakikisha kuwa unajitahidi kupunguza maadui. Fanya kila linalowezekana kuongeza marafiki ambao siku zote ndiyo nguzo muhimu nyakati za shida. Kumbuka kazi ya rafiki ni kufariji na adui kuangamiza!
Baada ya kusema hayo, naamini mada hii itawasaidia wengi, furaha yangu ni kusikia baada miezi, miaka michache kuwa watu wengi walijitegemea kutokana na hamasa waliyoipata kwenye soma hili! 
 


3 comments: