Tuesday, October 9, 2012

Woga una maana gani katika maisha? Angalia udhaifu wako hapa

Yawezekana unaposoma mada hii kuna jambo unaliogopa katika maisha yako. Huu ndiyo ukweli wa maisha ya mwanadamu kwamba woga ni sehemu ya uhai wake. Lakini umewahi kujiuliza msingi wa woga ni kitu gani? Jibu lipo kwenye makala haya. KATIKA hali ya kawaida tangu utotoni, mwanadamu amefundishwa kuogopa. “Acha usishike wembe utakukata!” woga humwingia mtoto na akaacha kuchezea wembe. Kila siku watu wanaogopeshwa mengi kwenye maisha yao. Lakini, kati yetu tumewahi kujiuliza tunaogopa nini? Kwa kuanzia, tutazame tafsiri ya neno WOGA kwenye kamusi ya Kiswahili. “Ni hali ya kuwa na hofu ya kufikwa na jambo la kutisha.” Hii ni maana ya kwanza, lakini ipo nyingine ambayo “ni hali ya kutoweza kustahimili vitisho.” Ukizama kwenye tafsiri ya kwanza unaweza kucheka kwa sababu watu wengi wanaogopa mawazo, fikra na wala si kitu halisi. Hebu angalia mwenyewe unachokiogopa kimekutokea au unafikiria tu kwamba kitakutokea na kujiuliza utafanyaje? Ukweli ni kwamba, kitu chochote unachokiogopa ni matokeo ya mawazo yako wala si hali halisi. Na kibaya zaidi udhaifu wako wa kutojiamini ndiyo unaokuogopesha zaidi. Ukichunguza kwa makini maana ya pili ya neno woga, unachokiogopa ni hali yako ya kutoweza kukabiliana na matukio yajayo. Maana si lazima kuogopa simba wakati una nguvu za kukabiliana naye. Si jambo la lazima kuuogopa moto kama una uwezo wa kupita katikati yake bila kuungua. Si lazima kitu fulani kikuogopeshe ikiwa unajiamini katika kustahimili vitisho vyake. Kumbuka; kila mtu mwoga ni mateka halisi wa mawazo yake na mwibiwaji wa ujasiri wake. Wengi wetu tutakuwa tunafahamu juu ya uwepo wa majambazi na wezi, ndiyo mana tunachukua tahadhari za kujilinda kwa kujenga kuta, kutembea na silaha na zana nyingine za kujilinda, lakini tumesahau kuwa mwizi wa furaha ni mawazo yetu hasi ambayo kila siku hutuambia kuna jambo litatushinda uwezo. Mwizi wa furaha yako atakufanya uogope mtihani hata kama umesoma usiku na mchana kujiandaa. Mawazo yatakuuliza maswali magumu, lengo ni kukufanya uogope, upoteze ujasiri , uondokewe na uwezo wa kustahimili na hatimaye ufeli kizembe kwa maswali uliyokuwa unafahamu majibu yake. Swali la kujiuliza ni kwamba unapimaje maumivu ya jeraha kabla hujaumia? Unakadiriaje aibu ya deni wakati hujashindwa kulipa? Unawezaje kutafunwa na simba wakati hajakung’ata? Ukiweza kumshinda kwa kumtia mateke woga wako utakuwa na maana gani? Ukiweza kujikinga lisikufike baya linalokuogopesha woga unaokusumbua ni wa nini kwenye maisha yako? Mpaka hapa utakuwa umenielewa kuwa unachokiogopa siku zote hakipo ila unakitarajia. Na matarajio ya woga husogea kila baada ya tukio fulani kukutokea. Unaweza kuanza kuogopa kupata ugonjwa wa Ukimwi, lakini ukiupata mawazo ya woga yatapiga hatua mbele, yatakufanya uogope kuumwa, ukiumwa, utaogopa kukonda, ukikonda utaogopa kufa. Sijui mtu akifa mawazo ya woga husogea wapi?

No comments:

Post a Comment