Monday, October 8, 2012

TOFAUTI KATI YA KUTAKA NA KUWA TAYARI KUPENDA

KATIKA ulimwengu huu tuna watu wengi wanapenda kuingia katika uhusiano wa kimapenzi. Ndani ya mapenzi kuna furaha, kusaidiana, ukamilifu wa ki utu na kutoshelezana kimwili. Hata hivyo, uchunguzi umeonesha kuwa, ipo tofauti kubwa kati ya mtu KUTAKA na kuwa TAYARI kuingia katika ulimwengu wa mapenzi. Ifahamike kuwa, watu wengi na hasa vijana wako kwenye ‘sayari’ ya kutaka kuwa na wapenzi kwa lengo la kutimiza tamaa zao za mwili. Wanataka kuwa na wenza ili wawasaidie kifedha, wapate mahali pa kutuliza hisia zao, wajikamilishe kwa upungu fulani wa kibinadamu na si vinginevyo. Kwa upande mwingine wataalamu wa mapenzi wanasema mtu aliye TAYARI kuingia kwenye mapenzi ni yule anayeongozwa na uzoefu, mwenye uwezo wa kuchuja kwa kina faida na hasara na kuamua kwa moyo wake wote kupenda. Mtu wa aina hii huwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za kimaisha na si mwepesi wa kuvunja uhusiano wake au kuyumba kimaamuzi. Fanya uchunguzi kwa kuwatazama wanaume/wanawake ambao wamefanya uhuni mwingi au kutamani kwa muda mrefu kuwa na wenza wanapopata nafasi huvumilia na kukabili matatizo mengi kwenye uhusiano wao. Uchunguzi huu unatufundisha kwamba, kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi na migogoro isiyoisha inatokana na watu wengi kuingia katika uhusiano kwa kutaka na si utayari ambao huambatana na akili kupevuka. Hebu jiulize kwa nini unampenda uliyenaye? Je ni kwa sababu anakupa fedha nyingi, anakutosheleza kwenye tendo, anakusaidia kwenye masomo au anakupa sifa mbele ya jamii kwa sababu ya umaarufu wake? Ukiwa na sababu hizo wewe ni mtu uliyeongozwa na matakwa na hivyo kuwa katika hatari ya kuumizwa au kujutia tamaa yako. Nakuomba uwe makini na KUTAKA kwako badala yake usubiri UTAYARI wa kuwa na mwenza wa maisha yako. Asante kwa kunisoma.

No comments:

Post a Comment