Wednesday, May 19, 2010

Hataki kunisamehe, naumia sana!




SWALI-Mimi ni msichana nina miaka 19 naishi Mwenge jijini Dar es Salaam, nasoma Chuo Kikuu. Nina mpenzi ambaye namchukulia kama mchumba wangu. Hivi karibuni alisafiri kwenda Gabon kikazi, aliporudi alikuja nyumbani kwetu lakini hakunikuta.

Akanipigia simu, nikamwambia niko kwa rafiki zangu nasoma. Tangu hapo alikasirika akinituhumu kuwa mimi si mwaminifu, nikimpigia simu hapokei na ameshaniambia kuwa hawezi kunisamehe. Binafsi sioni kosa langu, naumia sana naomba ushauri wako

JIBU-Mdogo wangu mapenzi ni utumwa wa hiyari utokanao na msukumo wa ndani ambao unaweza kudhibitiwa na mtu mwenye kuishi kwa kufuata nguvu ya utashi. Au kwa maana nyingine mapenzi ni ulevi ambao ukijiendekeza huwezi kuacha, lakini ukiamua unaweza. Ushauri wangu:

Wanaume matapeli wa mapenzi huwa hawakosi sababu ya kuvunja uhusiano. Sisemi umuone tapeli mpenzi wako lakini utambue hilo kwanza, ili usiwe mtumwa kwa kumpenda mtu asiyekupenda. Kinachokusumbua ni ulevi unaokufanya uamini kuwa mwanaume mzuri ni huyo tu akikuacha huwezi kupata mwingine, wakati si kweli!

Mdogo wangu, wanawake wanaofanikiwa katika maisha ya mapenzi ni wale wanaotambua thamani yao na kuyapa msukumo mafanikio ya maisha yao kwanza. Wewe unakosea kutanguliza suala la mapenzi kuliko maisha yako.

Nakupa angalizo kuwa inawezekana kabisa huyo jamaa unayemwita mchumba wako akawa wako ila wewe si wake, ndiyo maana ameamua kukuza sababu ndogo kuwa kubwa ili akuache. Unachotakiwa kufanya ni kujithamini, kujiamini na kutokuwa tayari kuwa mtumwa wa mtu.

Kwako mapenzi si kitu cha kwanza kwa wakati huu isipokuwa masomo ambayo ndiyo msingi wako wa maisha ya baadaye. Kwa kuwa umeshamuomba msamaha mpenzi wako naye hataki, inaonesha amekuchoka na namna yoyote ya kumfuata ni kujidhalilisha na kujitumikisha kwa mtu. Jipe moyo wanaume wapo wengi. JIAMINI.

No comments:

Post a Comment