Friday, October 19, 2012

Aliyetenda uovu anaweza kujitakasa mbele ya jamii?

“Nilipata mimba shuleni, wazazi wangu walikasirika sana, wakanisusa. Tangu hapo nimekuwa nikiwaambia nataka kusoma, wanasema hawawezi kumsomesha mhuni.” Msichana mmoja alinisimulia kisa hiki hivi karibuni. Baada ya simulizi hii nzito nilimtazama yule msichana kwa huruma. Nikamuuliza kama aliwaomba msamaha wazazi wake baada ya kosa lile? Alinijibu: “Niliwaomba lakini hawajanisamehe.” Yawezekana nawe msomaji wangu unapoungana nami kwenye mada hii ni miongoni mwa watu waliotengwa na jamii kwa sababu ya makosa yako. Maisha yako ya nyuma yalikuwa ya wizi na ujambazi kiasi cha kuwafanya hata ndugu zako wakutilia shaka unapowatembelea. Inawezekana ulikuwa kahaba, mkabaji, mtumia dawa za kulevya, mhuni ila kwa sasa umeachana na uovu wa aina hiyo lakini tatizo limebaki kwa jamii kuendelea kukuweka katika tabia ulizoachana nazo. Miaka kumi imepita tangu umeacha wizi lakini bado huaminiki, umebaki kujiuliza kwa nini jamii haikusamehe? Inakuwaje watu wanashindwa kubadilika sawa na uamuzi wako wa kuachana na ukahaba na badala yake wamebaki na picha ile ile ya maisha yako ya zamani? Katika hali ya kawaida, si rahisi jamii kusahau uhalifu wako na hasa kama wewe mwenyewe hujafahamu namna ya kusafisha madoa ya uchafu wako. Niko kwenye ukurasa huu kwa ajili ya kukushauri mambo ya kufanya ili uweze kujitakasa. Umfanye baba aliyekasirika baada ya kupata ujauzito akuamini tena. Umrejeshee imani bibi yako uliyemuibia miaka sita iliyopita akuchukulie tofauti na mwanzo. Angali dokezo zifuatazo. KUKIRI MAKOSA Watu wengi wanaponya uovu huwa wanaamini kuwa, wakiacha uovu fulani jamii itawaelewa na kuwasamehe moja kwa moja na hivyo kutoona umuhimu wa kukiri makosa mbele ya jamii, kitu ambacho si sahihi. Ukweli ni kwamba, kama umekuwa mkosaji wa hili na lile hakikisha unapoachana na tabia hiyo unarudi kwenye jamii au mtu uliyemkosea na kumuomba msamaha. Mwambie akusamehe kwa uovu wako na kumwahidi kutorudia tena, usikae kimya na kudhani atakusamehe hivi hivi tu. Anza kuishi maisha mapya yaliyo mbali na makosa. TANGAZA MABADILIKO Wakati unakusudia kuachana na uovu fulani uliokuwa ukiutenda, watangazie watu wakiwemo rafiki zako kuwa unabadilika kutoka kwenye tabia mbaya na kuishi maisha mema. Ukiacha bila kutangaza ni rahisi watu kudhani umepumzika tu kwa muda kuiba na kwamba siku zijazo utarudia hivyo kutokukuamini. TUMIKIA WEMA Sote tunajua matendo ndiyo yanayoweza kutafsiri tabia ya mtu kwa urahisi zaidi kuliko kitu kingine. Wengi huitwa malaya kwa sababu wanafanya vitendo vya ukahaba, wanaiba ndiyo maana wanaitwa wezi. Ukisema umeacha uhuni lazima ukate mizizi yote itakayokuhusisha na tabia hiyo na kutumikia uaminifu kwa vitendo. Ukifanya hivyo, baada ya muda jamii itakusamehe na kubaki na historia ya: “Alikuwa mhuni lakini amebadilika, enzi zake alikuwa mwizi, siku hizi ameacha. Asante!

No comments:

Post a Comment