Wednesday, June 23, 2010

Hofu ya kufa inanitesa, naomba ushauri
Naitwa Sakina naishi Tandale, Dar es Salaam, umri wangu ni miaka 23. Anko kwanza nakupongeza sna kwa ushauri wako, nimelazimika nikuombe ushauri kutokana na hofu ya kufa ambayo inanisumbua. Awali ya yote nilikuwa naendesha maisha yangu kama kawaida na sikuwa naogopa kufa kama hivi sasa.

Mwaka juzi alikuja msichana mmoja ambaye nilisoma naye Sekondari, akaomba tuishi wote, maana nimepanga chumba na sebule. Kifupi nilimkubalia kwa sababu na yeye alikuwa na mipango ya maisha yake, tukawa tunaishi kama ndugu na kufanya mambo mengi pamoja. Mwishoni kwa mwaka jana usiku tukiwa tumelala, rafiki yangu alianza kuugua tumbo ghafla, nilimkimbiza hospitali kwa ajili ya matibabu. Kusema kweli hakuchukua muda akafariki.

Tangu wakati huo Anko Rich nimekuwa naogopa kufa kuliko maelezo, kulala nashindwa naweweseka usiku na wakati mwingine natamani nitafute sehemu nijifiche maana naona kama umauti unanifuata kila niendako. Kusema kweli nakosa raha kiasi cha kushindwa hata kufanya mambo menngi ya kimaisha. Naomba unishauri kaka yangu nifanyeje?

Kwanza unatakiwa kuwa karibu na wataalamu wa masuala ya saikolojia na kuhudhulia kliniki ya nasaha kila siku, kwa wiki tatu au nenda kwa viongozi wa dini, lengo ni kukusaidia namna ya kuondokana na mawazo yenye kukuogopesha.

Fahamu kuwa hakuna mwanadamu ambaye haogopi kufa, lakini kiwango cha hofu kinatofautiana kutokana na ukubwa wa mawazo na hasa linapokuwepo suala la kuukataa ukweli. Ukiona mtu anaumizwa sana na tatizo lake, ujue kuwa anajiona kama hastahili kulipata na angependa kuona wengine wanapatwa na shida na si yeye. Lakini kwa wale wanaoona kuwa matatizo ni sehemu ya maisha, kiwango chao cha kusumbuka ni kidogo na mara nyingi hutafuta njia za kukabiliana na tatizo.

Ina maana wanapougua hawafikirii kufa, bali wanatafuta tiba ya kujiokoa wasife na kuweka matumaini yao kwa madaktari, dawa na hata dini zao. Wanapofanya hivi wanakuwa wanakabiliana na hofu kwa kushindana wakiamini wanaweza kukinga kifo. Mbinu hii ya kimawazo inafaa wewe pia uitumie na bila shaka itakusaidia kuondoa hofu.

Hapo ulipo unajitambua kuwa una hofu ya kufa, hebu jiulize nini kinakuua? Ukishakifahamu hicho kinachotaka kukuua, kabiliana nacho na uhakikishe kuwa tatizo hilo linaondoka. Ikiwa una ugonjwa, kuna kosa ulimfanyia mtu na unafikiri atakutoa uhai, tafuta suluhisho. Mwisho andika kila kinachokuogopesha na ukisome kila siku asubuhi kwa siku 90 utashangaa kitu hicho kinaenda kinapungua utisho na hatimaye utakiona ni cha kawaida. Kumbuka tangu tunazaliwa tunaogopa kufa mbona mpaka leo tupo? Naomba unione kwa msaada zaidi.

No comments:

Post a Comment