Tuesday, May 11, 2010

Njia nne za kufufua penzi lililochosha



Watafiti wa masuala ya kimapenzi tunaamini kwamba, mvuto wa mapenzi miongoni mwa wapendanao hupungua kadiri siku za uhusiano wao zinapokuwa nyingi, ushahidi unapatika kwa takwimu za usaliti kuwa chini ya asilimia 13 kwa mapenzi yenye muda wa kuanzia mwezi mpaka mwaka mmoja.
Inabainishwa kuwa kiwango cha watu kusalitiana hupanda sambamba na umri wa uhusiano wenyewe. Katika uchunguzi wangu nimebaini kwamba wanawake wengi hawasaliti ndoa zao katika kipindi cha uhusiano mchanga na kwamba huwa tayari kuvunja uhusiano na wapenzi wao wa zamani kwa lengo la kulinda penzi jipya.
Lakini upo ushahidi wa wengi kuanza kurejesha uhusiano waliokufa, pindi wanapoishi na wenza wao kwa muda mrefu kiasi cha kuzoeana sana. ( Nidokeze tu kwamba kuna wadanyanyifu wa mapenzi ambao husaliti ndoa hata siku ya harusi yao, hawa tutazungumzia habari zao wakati mwingine). Hali hii hutokana na kukinaishwa na penzi la wapenzi wao na hivyo kuhitaji mshawasha mpya.
Kushuka kwa msisimko wa kimapenzi kuna dalili nyingi lakini kubwa kati ya hizo ambayo ndiyo huwasumbua wengi hasa wanaume ni kushindwa kufanya tendo la ndoa na wenza wao au kutenda na kupata starehe chini ya kiwango. Kwa kipindi cha miezi minne nimepokea kesi zaidi ya 81 kutoka kwa watu mbalimbali zikieleza kuwa wamepoteza hisia za kimapenzi kwa wapenzi na wanandoa wao.
Jambo kubwa katika tatizo hili ni matokeo baada ya watu kupatwa na hali ya kupoteza hisia za mapenzi. Wengi wao wamekuwa wakiamua kuachana na wenza wao na kuanzisha uhusiano mpya kwa msukumo wa hisia kali za mapenzi machanga ambazo walikuwa nazo hata walipokutana na wale wanaoachana nao. Kitalaamu ukitafsiri uamuzi huo, unapata kasoro za ufahamu ambazo zinahitaji elimu.
Watu wengi wamekuwa wakiuliza, wanaweza kufufua penzi lililokinai? Jibu ni kwamba wanaweza, endapo watafuata mambo yafuatayo kwa vitendo. KWANZA ni kujenga ufamilia na umpendaye, nikiwa na maana kwamba awe rafiki na mtu wako wa karibu katika matembezi na maongezi. Wengi tunakutana na wenza wetu wakati wa kulala, sasa huo msisimko wa kimapenzi utapatikana wapi katika mazingira haya?
PILI, ni kumthaminisha mwenza wako kwa ubora kila wakati. Msisimko wa kimapenzi hauweza kuja kama hujavuta hisia juu ya jambo au maumbile fulani ya mwenza wako. Inashauriwa kila mara umtazame mpenzi wako kwa kumtathimini vema na kujivunia, miguu yake ya bia, umbo namba nane, kasheshe zake faragha na mvuto wake kwa ujumla. Ukiwa na vitu hivi vitakusaidia katika kuzalisha homoni na kukuza hisia zako.
Jambo la TATU ni kuwa na kitu kinachoitwa uchumi wa kimapenzi ambao hutokana na kumfikiria mpenzi wako kila mara unapokuwa kazini, kwenye matembezi na ikiwa unaona vitu barabarani au kwenye maduka jaribu kuwaza au kuvinunua kwa ajili ya kukuza penzi lako. Hapo utafanikiwa kukuza penzi.
NNE na la mwisho ni kuazima hisia. Kwa mfano unaweza usiwe na msisimko na mpenzi wako lakini ukawaza mwanaume mwingine na kumfananisha na uliyenaye, hili si jambo baya na linatajwa kusaidia kuamsha penzi lililokinai. Kama hilo halitoshi kuazima hisia kunakwenda mbali hadi kwenye kupokea sifa toka kwa rafiki zako zinazomhusu mwenzako, mfano. “Mume wako mpole anavutia kweli” Kauli hizi ukizitafakari zitakusaidia kufufua mapenzi yako.

No comments:

Post a Comment