Wednesday, April 7, 2010

UNAWEZAJE KUISHI BILA KUOGOPA KUFA?




Kama yalivyo magonjwa mengine auguayo mwanadamu, hofu ya kufa ni miongoni mwa magonjwa sugu yanayohitaji tiba. Ifahamike kwamba jamii husitisha kufanya majukumu yake katika kiwango cha kawaida endapo tu fikra za kufa zitakuwepo akilini mwao.
Kama rubani wa ndege atabaini kuwepo kwa shambulio la ndege yake aliyorusha au anayotarajia kuiruisha hatakuwa tayari kuendelea na safari na yuko radhi kutua kiwanja cha dharula kunusuru maisha.
Kunapokuwa na vita katika nchi yo yote ile, wananchi wake huwa tayari kujifungia ndani kwa kuogopa kuwa wakitoka nje watauawa. Hapa ina maana kuwa ujuzi wa kila mtu hufifia kwa sababu ya hofu ya kufa. Daktari atasahau wajibu wake na kiapo chake cha kufanya kazi kufa na kupona kunusuru maisha ya wengine na kuamua kwa furaha kubaki ndani na kuacha wagonjwa wakiteseka hospitali. Hali hadhalika waalimu, maijinia, wakulima nao watasalia majumbani kwa hofu ya kufa.
Kinachotokea baada ya mtu kuogopa kufa hali ya kuthubutu hupotea, si kwa sababu hawezi kufanya kazi zake au hana ujuzi, bali kuna ugonjwa umenyonya uwezo wake wa kufanya kazi. Ukweli huu hauna budi kufanyiwa mazoezi na kila mtu kwa lengo la kuondoa hofu hii mbaya kabisa.
Je katika maisha yako una ujasiri kiasi gani wa kukabiliana na hofu hii? Je ni watu wangapi ambao hudhubutu kutenda jambo mbele ya harufu ya kufa.
Baada ya kujiuliza hivyo tupige hatua katika kutafakari maswali mengine ambayo ni “wangapi kati yetu tunapenda kuishi? Ni maisha gani tunapenda katika kuishi kwetu ya raha au ya taabu? (Usisome maelezo yafutayo fumba macho utafakari na upate majibu kwanza).

Wakati naandika kitabu hiki niliwauliza maswali ya aina hii zaidi ya watu 20 wa rika tofauti, katika majibu yao 19 walisema wanaogopa kufa, ila wakachagua kuishi huku wengine kati yao wakipendelea kuishi maisha ya raha.
Tukubaliane na majibu niliyopata ambayo nadhani hata wewe msomaji wangu unapenda kuishi na pengine maisha ya raha kama walivyosema wengine waliotangulia.
Lakini kama uchaguzi wetu ni huo, basi lazima tufahamu kuwa tuna kasoro kwa kuwa tumeacha jambo moja la muhimu katika maisha ambalo lazima liambatane na utashi wetu huu mzuri tulionao. Tujiulize maisha mazuri ni yepi hapa duniani, je ni kumiliki gari, nyumba na vitu vya thamani?
Tupige hatua kwa kutafakari, tunawezaje kutumia vitu vizuri wakati tunaogopa kufa? Magari yanaua, umeme, chakula, dawa, usafiri wa ndege, mapenzi na kila tunachowaza kuwa ni moja kati ya kitu vizuri hakisimami peke yake bila kuambatanishwa na hatari ya kifo.
Je kwa mtazamo huu hatuoni kwamba tunataka kukwepa jambo muhimu lisilokwepeka katika maisha yetu? Kwa nini basi akili zetu zinashindwa kutambua kwamba kufa ni jambo la lazima ambalo kukimbia au kusimama hakututoi katika tatizo? Lazima tuamini kuwa hakuna mwanadamu atakayetoka salama katika vita yake na ulimwengu anaoishi, wote tutakufa.
Amelia Josephine Burr mwanafalsafa na mshairi wa Marekani aliyezaliwa mwaka 1878 na kupata heshima kubwa nchini mwake aliwahi kuandika “Beause I have loved life, I shall have no sorrow to die” Katika tafsiri isiyo rasmi anasema: kwa kuwa amependa kuishi hahuzuniki akifa. Hii ni falsafa ya hali ya juu sana ambayo ina mwanga wa mafanikio kwa kila mwanadamu atayekichukulia kifo kama sehemu ya furaha ya maisha yake.
Katika kutafuta mafanikio ya maisha haya mwanadamu hawezi kufikia kiwango cha juu kama kutafuta kwake hakukuambata na furaha ya kufa. Mkulima alime kwa kiapo cha kufa, wafanyakazi, watafiti, wanasiasa wanaotaka kufanikiwa katika kazi zao lazima wajitolee kufa, la sivyo kifo kikitawala fikra zao uwezo wao wa kufanya kazi utashuka na hakutakuwa na mafaniko.
Watu wengi siku hizi wanafikiria zaidi kuhusu uchawi kazini, nyumbani na kujikuta wanapunguza kasi kiutendaji kwa kuhofia kwamba watauawa. Hivi kujitesa huku kuna maana gani katika maisha? Nimewahi kusikia watu wakikataa kuvaa vizuri, kujenga nyumba, kuonekana wenye pesa katika jamii kwa hofu ya kuuawa?
Ni lazima tubadili kwanza mtazamo kuhusu kifo kama tunataka kusonga mbele katika maisha yetu. Watu wanaoogopa kufa hufanya kazi kizembe kwa kupunguza uwezo wao na matokeo yake hukwama kufikia malengo waliyojiwekea na kudhani mambo hayawezekani kumbe hawakutenda ipasavyo.
Winston Churchill mwanasiasa mashuhuri nchini Uingereza aliyepata kuwika kati ya mwaka 1940-1945 aliwahi kusema kwamba: “success is the ability to go from one failure to another, with no loss of enthusiasm." Au kwa maana nyingine mafanikio ni uwezo wa kusonga mbele kutoka kwenye kushindwa kwa mara ya kwanza na kuendelea bila kupoteza hamu ya kujaribu.
Kwa maana hiyo kama tutachukulia kushindwa kama changamoto na kufa kama jambo la lazima lisilokuwa na madhara tutafanya kazi kwa kiwango cha juu na bila shaka tutapata ushindi mkubwa katika majukumu yetu.
Aidha baada ya kufahamu kuwa maisha na kifo ni vitu pacha, tusonge mbele katika kutazama namna gani tunaweza kuepukana na hofu hii? Kwanza ni kuacha kuweka alama katika akili zetu kwamba kifo ni jambo la hatari na kama tulishaweka basi hatuna budi kuacha kuitumikia hofu hiyo kwa kuamini kwamba kufa kupo na siku moja lazima tutakufa.
Kuna mtu mmoja alikwenda kwa doktari na kumwambia kuwa “Dokta mimi niko karibu kufa kutokana na kwamba napata maumvu makali sana ninapokigonga kichwa changu kwenye ukuta” Dokta alimwambia: “ili usife usigongeshe kichwa chako kwenye ukuta na maumivu hayatakutokea tena.”
Hivyo basi kama tuna hofu ya kufa tuache kuogopa, usiidhuru miili yetu kwa hofu isiyokuwa na sababu. Mimi huwa sielewi kwa nini wagonjwa wa kansa, ukimwi kifua kikuu, moyo, kisukari wengi wao huwa na hofu sana ya kufa? Je ni kweli kwamba wanaokufa ni wagonjwa tu, mara ngapi wamekufa watu katika ajali? Bila shaka kuwaza kifo kwa sababu tu ya kuumwa nao ni utumwa wa mawazo wa kujitakia.
Ni lazima tufanye kazi zetu kama watu tutakaoishi milele na kifo kiwepo katika akili zetu kama muongozo wa umakini katika kutekeleza majukumu yetu si kizuizi cha kutufanya tuogope kufanya jambo kwa hofu kwamba tukifanya zaidi ya uwezo wetu tutakufa.
Mambo yote yanayotuzunguka yana harufu ya kifo, hivyo hatuwezi kukwepa. Tufahamu kuwa kazi zetu, biashara, miradi, na kila tukifanyacho kinakufa pia tukiogopa hatutaweza kufanya jambo lo lote. Mwisho kwa wenye imani za dini ni vema wakasali sana katika hatua za kukabiliana na hofu hii mbaya huku wenye kujiamini wenyewe nao wakifanya hivyo!

No comments:

Post a Comment