Wednesday, April 7, 2010

SIFA KUMI ZA MPENZI WA KWELI





Mpenzi msomaji wangu, ni wakati mwingine ambao tunakutana katika uwanja huu wa maisha na mapenzi, kwa lengo la kujifunza namna ya kuwa wapenzi bora. Sina shaka tumemaliza salama siku yetu ya wapendanao, ingawa naamini kuna wengine wamemaliza kwa kilio maana siku hizi ni fasheni kuachana.

Vijana wengi ambao wanapendana leo mapenzi yao hayadumu kiasi cha kubatizwa jina la utamu wa bazoka. Lakini yote hii inatokana na ukweli kwamba elimu ya mapenzi ambayo ni muhimu kwa binadamu haitolewi ipasavyo.

Ipo zana potofu kwamba kumfundisha mtoto mapenzi ni kumharibu, jambo ambalo si kweli bali inategemea mtoto huyo anafundishwa nini na kwa wakati gani. Lakini cha kushangaza zaidi hata watu wazima ambao ni wadau wa mapenzi hawayajui, matokeo yake wanajiingiza kwenye uhusiano wakiwa bumbumbu na hivyo kuteshwa na changamoto zinazowakabili.
Leo tutajifunza kwa undani sifa kumi za mpenzi bora ili tuweze kuwatambua wapenzi wetu kabla ya kuwapa mioyo na utu wetu. Sifa hizo ni hizi zifuatazo.

KWANZA: Mpenzi wa kweli ni yule ambaye hatangoja kujua nini unahitaji yaani hana sababu ya kusubiri kuombwa ndiyo atoe msaada.

PILI: Ni yule atakayejua wakati gani huna furaha au una furaha na atakuwa na wewe kwa hali zote mbili .

TATU: Ni yule atayekuwa tayari kukusikiliza kwa kile utakachosema, hatojali umeongea baya au zuri .

NNE: Atakuwa na wewe wakati wa shida na raha. Hatakuwa mtu wa kuvizia vizia na kujisogeza wakati ukiwa na raha.

TANO: Mpenzi wa kweli atakuheshimu na hatopenda kuwa kikwazo cha maisha yako, atakulinda daima.

SITA: Atakupenda kwa moyo wake wote na wala si kwa ajili ya shinikizo fulani (pesa au mali)

SABA: Mpenzi wa kweli ni yule atakayeonyesha kuthamini nafasi yako kama rafiki au mpenzi mbele ya wengine, hafichi hisia zake mbele za watu, atakutetea na kukufanya wa kwanza.

NANE: Kwenye ukweli mpenzi mzuri atasema bila kukuficha na atapenda kukuonyesha mifano ya namna ya kuwa mkweli na mwaminifu.

TISA: Mpenzi wa kweli ni yule anayejiamini, asiyeyumba katika maamuzi hata kama atalazimika kufanya maamuzi magumu .

KUMI: Atakuwa tayari kuvumilia, hatakuwa mwepesi wa hasira wala kutumia lugha chafu na ubabe.
Naomba leo niishie hapa, ukiwa na mwaswali nipigie au tembelea website yangu ya www.manyota.webs.com .

No comments:

Post a Comment