Wednesday, April 7, 2010

AINA KUU NNE ZA MAPENZI DUNIANI




Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kuna aina nyingi sana za mapenzi miongoni mwa binadamu. Hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kupenda kwa mtu mmoja au watu kadhaa hakuwezi kulinganishwa na wengine kwa mazingira na mienendo.

Wakati fulani niliwahi kufanya uchunguzi miongoni mwa wapenzi ambapo nilikuwa nawauliza swali. “Vipi dada/ kaka, huyu ni mpenzi wako?” Wengi kati ya niliowauliza hawakupoteza hata nusu sekunde kujibu ‘NDIYO’.

Lakini watu hao hao nilipowauliza kwa mara nyingine “Unampenda kwa sababu gani?” Majibu ya wengi yalikuwa na sababu ambazo si za msingi na wengine walinyamaza au kuambulia kucheka.

Hebu wakati tunaendelea na mada hii, jiulize wewe mwenyewe ambaye una mke/mume swali kama hilo unampendea nini huyo mpenzi wako? Baada ya hapo sababu zinaweza kuwa ni kama zifuatazo “ Nampenda kwa sababu ni mzuri wa sura, tabia, umbo, na kusema kweli ananivutia” la kama hizo hazitakuwa sababu sina shaka nawe utanyamaza au utacheka.

Hii ina maana kuwa watu wengi ambao tuna wapenzi iwe wake au waume zetu, huenda tuliwapenda au tunawapenda hadi sasa bila kufahamu kwa nini tunawapenda na kitu gani kilitufanya tuwe wapenzi. Maana ikiwa ni uzuri, tabia, mvuto na sababu nyinginezo, basi lazima tufahamu kuwa uhai wa mapenzi yetu ni mdogo.

Inasemwa hivyo kwa sababu watu hubadilika tabia, sura, umbo, mvuto, ufahamu na hivyo kuweka ukomo wa mapenzi kuwa ni baada ya kutokea kwa mabadiliko hayo ambayo ni ya kawaida katika maisha ya mwanadamu, kwani ni wazi kwamba hakuna kinachodumu miongoni mwa hivyo vinavyotajwa na wengi kama sababu za kupendana.

Watalaam wa elimu nafsi na hasa Bw. Robert Stenberg walijitahidi sana kufanyia utafiti wa mapenzi na kuibuka na aina kuu kiasi cha nne ambazo wanazitaja kuwa ni PENZI LA UTIIFU, PENZI LA KUJALIANA, PENZI LA UIGIZAJI NA PENZI TIMILIFU.


Ufafanuzi unaotolewa na wataalamu hawa unaonyesha dhahiri makosa yanayoweza kufanywa na binadamu katika kuchagua au kupata wapenzi. Jambo ambalo limepelekea kuporomoka kwa uhusiano mwingi kati ya wanaume na wanawake. Wanasema penzi kamili linatakiwa kuwa na sifa tatu, ambazo ni tendo la ndoa, ukaribu na kujitolea.

PENZI LA UTIIFU

Penzi la utiifu au kama wengi wanavyolifahamu hujulikana kama ‘penzi la mahaba’. Katika aina hii ya penzi, wanaopendana hujali sana na kuendekeza zaidi miito ya kimwili. Mapenzi ya kiwango cha juu kabisa miongoni mwao hupatikana pale wanaposhiriki tendo la ndoa. Pia wanaopendana hupenda kuwa pamoja au karibu kwa muda mwingi.

Lakini kwa bahati mbaya penzi la aina hii linakosa sifa moja ambayo ni kujitolea. Wapenzi kwenye penzi hili huonekana na pengine hujiona kuwa wanapendana, lakini unapofika wakati ambapo kujitolea kunahitajika, penzi lililoonekana kushamiri hupukutika ghafla.

Kujitolea kunaweza kuwa na maana ya kuumia kwa ajili ya mwingine, kutoyumbishwa na watu wa pembeni na kuwa tayari kulinda penzi hilo kwa gharama yoyote. Kwa mfano ukiona mpenzi wako hayuko tayari kukusaidia unapoumwa, unapokuwa na matatizo, hakuhurumii unapokuwa taabuni ujue kuwa mapenzi yenu ni ya utiifu ambayo uhai wake ni mdogo.

Jambo la kufanya hapa ni kwa wapenzi wenyewe kujitambua na kuchukua hatua za kukamilisha pengo la kujaliana ili kutowapa nafasi wambea na shida za dunia kuyumbisha meli ya penzi ambayo wanasafiria, ikishindikana watu hawa wanashauriwa kutokuwa wepesi wa kuoana kwani uwezekano wa ndoa yao kutodumu ni mkubwa.

PENZI LA KUJALIANA

Penzi la kujaliana ni lile ambalo wanaopendana wanakuwa karibu mara zote na kushiriki mambo mengi pamoja. Wapenzi wa kundi hili huwa na hali ya kujitolea tofauti na penzi la utiifu ambalo tumeliangalia, lakini kasoro yao kubwa huwa kwenye miito ya mwili. Jambo la kufurahisha hapa ni kwamba wapenzi wa kundi hili wako makini kwa kila sehemu na mara nyingi huwa hawakubali kuingiliwa maamuzi ya mapenzi yao.

Lakini linapokuja suala la tando la ndoa hujitokeza kasoro nyingi za kutofikishana kileleni au kutofurahishana na hivyo anguko lao huletwa na muwasho wa mwili ambao huwasukuma wapendanao hao kutoka ndani ya uhusiano wao na kufanya usaliti.

Sasa ili kulifanya penzi la aina hii liwe imara lazima wapenzi waulizane kuhusu kutimiziana haja za mwili wanapokuwa faragha. Kama kuna kasoro kati yao si busara kufichana wanatakiwa kuwaona wataalamu wa mapenzi na kupata ushauri utakaosaidia kuondoa tatizo hilo. Hawa pia wanashauriwa kutooana haraka.

PENZI LA UIGIZAJI

Penzi la aina ya tatu linalotajwa na watafiti ni lile lijulikanalo kama penzi la Uigizaji. Hili ni lile penzi ambalo wanaopendana hukutana asubuhi na ikifika jioni tayari ni wapenzi kamili, ambapo hugandamana kama ruba, utadhani waigizaji wako kwenye matayarisho ya filamu. Ukiwatazama wanakuwa kama vichaa na msukumo wao wa kutimiza hisia za mwili huwa ni mkubwa kiasi cha kufikia kufanya mapenzi hata barabarani au kwenye sehemu za wazi.

Wapenzi wa aina hii huchukua muda mfupi sana kutangaziana mambo ya ndoa na pengine kuoana bila kufahamiana zaidi kitabia. Wanajuana asubuhi na jioni mwanamke/mwanaume keshahamia kwa mwenzake na maisha yanaanza, hapo hakuna ushauri wala muongozo wa watu wengine.

Tatizo kubwa ambalo hujitokeza katika penzi la aina hii ni wapenzi kuchokana mapema na hamu ya kufanya tendo la ndoa kupotea. “Yaani nikiwa na mume wangu sijisikii kabisa kufanya naye mapenzi, lakini kwa wengine nakuwa na hamu sana” hizi ni kauli za wapenzi wa penzi la kisinema sinema.

Mbali na hilo wapenzi wa aina hii ni rahisi kuporwa na kuanzisha uhusiano mpya, hivyo inashauriwa kuwa kwa wale ambao wanaona kuwa wako kwenye kundi hili, wajitahidi kujizuia na kupeana nafasi za kujuana zaidi kupitia ushauri wa watu wengine. Si vema kushiriki tendo la ndoa kila mara kwa staili na sehemu zile zile na pia haifai kukurupuka kuoana bila kuchunguzana tabia, ndoa za hivi hazidumu.


PENZI TIMILIFU
Aina ya mwisho ya penzi kama inavyoelezwa na mtaalamu Sternberq ni ile ya penzi timilifu. Aina hii ya mapenzi inakuwa na sifa zote tatu, yaani TENDO LA NDOA. Kwamba wapendanao huwa hawana kasoro katika eneo hili, unapofika muda wa kupeana raha hufikishana mahali pa juu. UKARIBU kwamba muda wote huwa karibu na kila mmoja hakai na kiu ya kutokumuona mwenzake kiasi cha kupoteza hisia na kushawishika kufanya usaliti.

Sifa ya mwisho ni KUJITOLEA. Ni mahodari kusaidiana, kufarijiana na hawako tayari kupokea mambo kutoka pembeni yanayohusu uhusiano wao, hivyo huwa si rahisi kwao kuyumba kwa sababu za umbea. Kumbuka katika penzi hili tendo la ndoa huwa si sehemu muhimu sana kwa wapenzi, yaani kwao penzi ni rohoni zaidi kuliko mwilini hata wakikaa muda wa miezi mitano bila kufanya tendo la ndoa upendo wao haupungui.

Hata hivyo, penzi la aina hii kwa mujibu wa wataalamu ni vigumu kupatikana na ni vigumu pia kulilinda, lakini linatajwa kuwa ni aina ya penzi bora ambalo ni muafaka kwa maisha ya baadaye ya ndoa kwa wanaopendana. Watu wengi kwa kutotambua aina hii ya mapenzi wamejikuta wakiliharibu kwa kufikiri tu kwamba wapenzi wao wamefika na hivyo kufanya makusudi ya kuharibu misingi ya penzi.

“Nimeshamshika atakwenda wapi, nikikohoa tu anaitika” Kauli kama hizi ni hatari sana katika penzi hili, hivyo inashauriwa ukiona unapendwa na mpenzi wako katika aina hii ya penzi ni vema ukawa macho ili kutolivunja kwa uzembe wako na kudhani unababaikiwa kumbe unapendwa kwa dhati.

3 comments: