Wednesday, April 14, 2010

Faida za utii na uaminifu kwa mwanafunzi




Nguzo imara ya mwanafunzi yeyote anayetaka kufanikiwa katika masomo yake ni kuwa mfuasi wa UTII na UAMINIFU mahali popote na kwa mtu yeyote. Nakumbuka wakati nikiwa shule ya sekondari nilikiuka sana mambo haya muhimu, nilikuwa mtu wa vurugu na mwanzilishi wa migomo.

Wakati huo sikuona kama nilikuwa nafanya makosa, mara zote nilijitazama kama shujaa kwa vile jamii, walimu na wanafunzi wenzangu walikuwa wakiniogopa. Kifupi nilikuwa na akili darasani lakini matokeo ya mwisho yalipotoka yalinishangaza kwani nilifeli.

Kushindwa huko kulinirudisha kwenye mikono ya wazazi ambao tayari nao nilikuwa nimewachosha kwa tabia zangu. Toka hapo hakuna mjomba wala shangazi aliyejitokeza kunisaidia kimasomo kwa kuwa sikuwa mtu wa kuaminiwa. Nilikaa nyumbani kama mtu muhuni kwa miaka mitano hadi nilipokubali kubadili tabia yangu.

Nilifikia uamuzi huo kwa sababu nilinusurika kufungwa jela baada ya kushiriki katika ugomvi ulioleta harufu ya mauaji ya kijana mmoja tuliyekuwa tukigombana naye. Nililazimika kutoroka na kukaa uhamishoni kwa miaka kadhaa. Baadaye nilikutana na maisha magumu ambayo siwezi kuyasahau.

Nakumbuka wakati huo wa dhiki nilijutia utundu nilioufanya shule kwa kuchezea elimu na kujikita katika mambo ya kihuni ambayo hayakunisaidia. Mwezi wa nane mwaka 1998 nilikubali kubadilika na kuanza kujifunza upya maisha ya utii na uaminifu chini ya uongozi wa walimu wa dini yangu ya kikristo.

Mafundisho ya kidini yalinisaidia kuacha ulevi na uvutaji wa sigara. Marekebisho hayo ya tabia yalinijenga zaidi upande wa rafiki zangu niliokuwa nasali nao, lakini ndugu walikuwa bado wananitilia shaka. Rafiki zangu hawakupata shida tena kunituma kusimamia ujenzi wa nyumba zao na miradi yao na mara nyingine niligeuka kuwa ‘benki’ nikawa natunza pesa za watu.

Simulizi ni ndefu lakini mwisho wa yote uaminifu wangu huo ndiyo uliomsukuma mmoja kati ya rafiki zangu kujitolea kunisomesha masomo ya jioni ili nirudie masomo niliyofeli nilipopata nafasi hiyo sikuichezea kwani tayari nilikuwa nimeonja machungu ya ujinga. Nilijituma kusoma kwa malengo na kufanikiwa kusahihisha cheti changu.

Nilipomaliza nilichagua fani ya uandishi wa habari, ambapo alitokea mama mmoja niliyemheshimu na kumtii akanisaidia tena kunisomesha. Kifupi maisha yangu yalikuwa ya kubebwa na watu niliowaonesha uaminifu na utii wangu.

Hawa ni rafiki zangu wa hapa nchini achilia mbali Dr ………………… kutoka chuo cha American Psychology ambaye alijitolea kunifundisha masomo ya Saikolojia elimu ambayo ilinifumbua macho na kuniwezesha kuwa hivi nilivyo sasa.

Huu ni ushuhuda wangu kwa ufupi, ambao nimeutoa kwa lengo la kuwafundisha kwa vitendo nguvu ya uaminifu na utii katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na hasa kwa wanafunzi ambao safari ya kupata elimu inahitaji ushirikiano wa watu wanaoishi nao nyumbani na shuleni.

Wanafunzi wengi wameshindwa kufanikiwa kwa sababu ya kutokuwa waaminifu na watii kama nilivyoeleza huko nyuma, jambo ambalo limewafanya watengwe na jamii mithili ya yale yaliyonitokea mimi.

Ifahamike kuwa mwanafunzi hawezi kupata msaada wa kutosha kwa wazazi, walimu na ndugu zake kama atakuwa akipewa ada anaitumia vibaya, akiwa na kashfa za ngono, wizi, uvutaji bangi na utumiaji wa dawa za kulevya na kuonesha ukorofi.

MADA HII INAENDELEA UNAWEZA KUIPATA KWA KIREFU KAMA UTANUNU KITAMBU CHANGU CHA SAIKOLOJIA MBINU 100 ZA KUSOMA NA KUFAULU MITIHANI. KINAUZWA NA WAUZA MAGEZETI NCHI NZIMA

No comments:

Post a Comment