Wednesday, April 16, 2014

Namna ya kuzungumza na aliyekukasirikia

 Kwenye maisha kuna nyakati za kutofautiana, kukasirishana. Katika hali ya kawada kipindi hiki huwa ni za hatari kwa sababu husababisha nyufa kubwa za uhusiano katika jamii.
Sote tunajua, watu hupigana, huachana, hujeruhiana, hutukanana, hudhalilishana wakiwa na hasira. Hata hivyo, si wote wanaojua wafanye nini wanapojikuta wameingia kwenye hatua hiyo mbaya.
Msomaji wangu, hebu jaribu kukumbuka ugomvi mmoja uliotokea kati yako na mwenzako na ikiwezekana jikumbushe mlivyoanza! Utabaini kuwa mlianza kama utani na mkajikuta mmefura kwa hasira, mkatwangana makonde, mkatamkiana maneno makali ya kuudhi na pengine mkafikia uamuzi mbaya.

Yote hii ni kwa sababu mlikosa elimu ya mazungumzo. Ingekuwa mmoja wenu hasa yule aliyekuwa wa pili kukasirika anafahamu hatua za kuzungumza na mtu aliyekasirika angechukua jukumu la kutuliza machafuko na kuleta amani kwenye jamii. 
Ungana nami leo katika kutafakari hatua zifuatazo zinazoweza kusaidia kuzungumza na mtu aliyekasirika.

MPUNGUZE MHEMKO
Hasira hujaza kifua, huathiri mzunguko wa damu na ufahamu. Mtu aliyekasirika  huwa vigumu kwake  kusikiliza au kutazama mambo kwa jicho la tatu. Mwenye hasira huwa hafikirii matokea yajayo badala yake hutazama zaidi tukio na jinsi ya kupata ushindi iwe kwa maneno au kwa mapambano.
Katika hali ya namna hiyo, mtu mwingine akija na busara za kutaka kumgeuza haraka haraka hawezi kumuelewa. Muhimu hapo ni kuacha kumwadama, kujibizana naye, kumshawishi asikilize badala yake mpe nafasi ya kusema atakavyo, abwate ajuavyo huku wewe ukimuitikia na kumkubalia lawama zake. “Basi ndugu yangu mwenye makosa ni mimi.” Kauli za aina hii zitampunguza hasira kwani atajiona msindi.

MSOME SAIKOLOJIA YAKE
Kwa kumfahamu mpenzi/ndugu yako kwa kina itakuwa rahisi kwako kumtambua kuwa amepunguza hasira na kurudi katika hali yake ya kawaida. Ukisha fahamu hilo chukua jukumu la kumsoma kisaikojia ili kujua kama yuko kwenye hali nzuri ya kusikiliza yale uliyotaka kumwambia wakati alipokuwa na hasira.
Zoezi hili linaweza kuchukua saa kadhaa na wakati mwingine hata siku mbili. Lengo ni nini? Ni kupata matokeo sahihi ya kuondoa chuki za mwenzako na kumfundisha madhara ya kukasirika. “Ndugu yangu nakupenda sana, lakini juzi uliniumiza, uliniambia mimi malaya kwa kosa ambalo sikufanya?” Bila shaka muda huo atakusikiliza zaidi kuliko ungebishana naye  alipokuwa na hasira.

MRUHUSU AKUJIBU
Pamoja na kumsoma kisaikojia na kumwambia kinagaubaga makosa yake, usimzuie kujitetea, mpe nafasi ya kuzungumzia kilichomkasirisha. “Unaona bado unanitukana, sasa naamini siku ile ulikuwa umedhamilia.” Usisiseme hivyo, mwache ajibu hoja hata kama atakuwa anakukandamiza na kuzidi kujijengea ushindi. Mvumilie aoshe ubongo wake.

EPUKA MARUMBANO
Kama nilivyosema hapo juu wengine huwa wagumu kuelewa, ni watu wa kuficha udhaifu wao na kutopenda kuonekana wamekosea. Watu wa namna hii unapowarejeshea mazungumzo  wanaweza kujikuta wanahamaki tena.
“Kwa hiyo ulikuwa unasemaje…nilifanya ndiyo,… wewe unaamuaje?” Mkifika kwenye alama hiyo usikubali kurumbana naye mwache aseme halafu wewe ingia kwenye hatua ya tano.

MUOMBE MSAMAHA
Hata kama atakuwa yeye ndiye mwenye makosa na amekataa kukiri, usijali, chukua jukumu la kumuomba msamaha na kueleza tena nia yako ya kumazungumzo ilikuwa ni kuelewana si kugombana. Kumbuka hata kama amekiri kosa, bado unatakiwa kumuomba radhi kwa kurejea yaliyopita. “Ndugu yangu inawezekana nikawa nimekuudhi tena kwa niliyosema, nakuomba sana tusameheane.”
Bila shaka kwa haya machache msomaji wangu utakuwa umejifunza na kuchukua hatua za kuzuia migogoro mikubwa inayotokana na hasira. Katika maisha tusikubali kuruhusu hasira zitumike kutuchumia janga la majuto.

No comments:

Post a Comment